Mkuu wa Mkoa Singida Dk. Binilith Mahenge akihutubia Wafanyakazi katika Sherehe za Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi iliyofanyika kimkoa katika Uwanja wa Namfua (Liti), Manispaa ya Singida jana.
Wafanyakazi wakiwasili uwanjani wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali na kuonesha idara wanazotoka ikiwa ni kusheherekea kilele cha maadhimisho ya sikukuu hiyo.
Wafanyakazi wakiimba wimbo wa Mshikamano ktika kilele cha maadhimisho ya sikukuu hiyo.
Kikundi cha ngoma za utamaduni cha Mbalamwezi cha Manispaa ya Singida kikitoa burudani katika sherehe hizo.
Kaimu Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Hamisi Mtundua akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na wafanyakazi.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKISHO la vyama vya Wanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Singida limesema kutowatimizia wafanyakazi stahiki zao kunawasababishia kukosa ari ya kufanyakazi kwa juhudi.
Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Singida, Susan Shesha ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Singida wakati akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa Dk.binilith Mahenge katika maadhimisho ya sherehe ya wafanyakazi duniani iliyofanyika jana kimkoa Uwanja wa Namfua (Liti)
“Nitaje baadhi ya mambo hayo yanayofifisha ari ya wafanyakazi kushindwa kufanya kazi kwa juhudi kuwa ni kutopata nyongeza ya mshahara kwa muda mrefu, shirika la bima kutowalipa watumishi waliokata bima ya maisha pindi bima zao zinapoiva hivyo kupelekea malalamiko mengi kwa watumishi waliojiunga na bima hiyo” alisema Shesha.
Alitaja mambo mengine kuwa ni madai ya fedha za uhamisho, likizo pamoja na malimbikizo ya mishahara kucheleweshwa hadi wengine kustaafu, baadhi ya wakurugenzi kutohuisha mabaraza ya wafanyakazi kwa wakati, waajiri wengi wa sekta binafsi kutojua sheria ya ajira na mahusiano kazini, sheria ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi na sheria ya usalama mahala pa kazi na waajiri binafsi kutowasilisha makato ya asilimia 10 kwenye mfuko wa Hifadhi ya Jamii changamoto ambayo uwakumba wafanyakazi wa sekta binafsi na kuwafanya wasione umuhimu wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii.
Shesha aliendelea kutaja sababu zingine kuwa ni bima ya afya kuchagua baadhi ya dawa kulipia kwa makato ya bima, kutoundwa kwa bodi ya kima cha chini cha mshaahara,kutotolewa kwa huduma ya afya kwa wanachama wastaafu kutoka mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa kwa sekta binafsi, kutohimitishiwa kikamilifu zoezi la watumishi wa umma wa darasa la saba waliositishiwa ajira zao, makato ya ya bodi ya mikopo ya Elimu ya juu yazingatie mikataba ya wanufaika na waajiri kutopeleka michango ya hifadhi ya jamii kwa wakati hivyo kupelekea tozo kubwa na kusababisha wastaafu kuchelewa kupata pensheni zao.
Katika risala hiyo watumishi hao walitoa baadhi ya maombi yao kwa serikali kuwa nyongeza ya mishahara iendane na hali ya uchumi wa sasa, uhamisho wa watumishi uendane na ulipwaji wa stahiki zao kwani kuendelea kuhamisha bila malipo kunapingana na taratibu za utumishi na wanaiomba Serikali ilipe madeni ya watumishi kwa wakati ili kurejesha imani ya watumishi kwa Serikali yao.
Mambo mengine walioomba ni waajiri wa sekta binafsi watoe mikata mikataba ya kudumu kwa wafanyakazi, likizo na kima cha chini cha mshahara kizingatiwe, mabaraza ya kazi yafanyike kwa wakati na malipo ya posho yatolewe kwa mujibu wa sheria na isiwe hisani ya mwajiri, wafanyakazi wanaolipwa kwa mapato ya ndani (GF) walipwe mishahara yao kwa wakati na malipo ya wastaafu yalipwe kwa wakati.
Shesha alisema maombi yao mengine ni kodi kwenye mishahara iendelee kupunguzwa, baadhi ya waajiri, viongozi wa serikali na kisiasa wenye tabia ya kuwaadhibu watumishi bila kuzingatia sheria na kanuni za utumishi kuacha kufanya hivyo ambapo walimuomba mkuu wa mkoa ofisi yake itilie mkazo kwa wajiri ambao hawataki kuchangia katika sherehe za Wafanyakazi Mei Mosi.
Akizungumzia mafanikio waliyopata ni waajiri kutoa fursa kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi kutimiza majukumu yao bila kubughudhiwa, ushirikiano mzuri wa vyama hivyo na waajiri hasa wakurugenzi wa katika halmashauri, kuendelea kuwa na amani katika nchi kumezidi kuchochea ufanisi kazini kwa sababu wafanyakazi hufanya kazi bila hofu.
Aidha Shesha alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwapandisha madaraja watumishi na ulipwaji wa malimbikizo yao waliyokuwa wakidai.
Dk. Mahenge akizungumza baada ya kupokea risala hiyo alisema mambo yote yaliyondani ya uwezo wake atayafanyia kazi na yale ya kitaifa yatapelekwa kwa wahusika ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuiletea nchi maendeleo.
Alisema Serikali imefanya kazi kubwa mno ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kwa mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Mkoa wa Singida ulipewa Sh.232 Bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mirad imbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko aliwaambia wafanyakazi hao kuwa baada ya sherehe hiyo waende wakafanye kazi kwa bidii na kwa ‘ step’ kama walivyokuwa wakicheza vizuri kwaito na si vinginevyo.
Kaimu Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Hamisi Mtundua akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na wafanyakazi alishukuru Serikali kwa kazi kubwa iliyoifanya mkoani hapa ya miradi mbalimbali kama ujenzi wa vituo vya afya, miradi ya maji, ujenzi wa madarasa, ujenzi wa zahanati, barabara na umeme.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa Dk. Binilith Mahenge kwa kazi nzuri anayoifanya mkoani hapa na kusimamia utelekezaji wa miradi hiyo kwa uaminifu mkubwa kwa kushirikiana na watendaji wake wakiwemo wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa wilaya na watumishi wa kada mbalimbali.
Katika sherhe hizo watumishi waliofanya vizuri walitunukiwa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu na Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ilitangazwa kuwa ya kwanza kwa kuongeza fedha za zawadi kutoka Sh.300,000 hadi Sh.500,000 huku Wilaya ya Itigi ikiibuka mshindi kwa kushika nafasi ya kwanza ikifuatia Ikungi kwa kuwajali watumishi na ushirikiano mkubwa wanaovipa vyama vya wafanyakazi mkoani hapa na kuwa halmashauri bora ambazo hazina malamiko makubwa ya watumishi kwa kuwatendea haki.
Wafanyakazi Mkoa wa Singida wamezipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Itigi na Ikungi kwa kuibuka kidedea na kuwa waajiri bora kwa mwaka 2021/2022 ambapo wameziomba halmashauri zingine kuiga utendaji kazi wa halmashauri hizo.