Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza Ramadhani Ng’anzi akizungumza na wandishi wa habari juu ya namna walivyojipanga kuimarisha ulinzi kwenye sikukuu ya Eid El Fitri
****************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza limejipanga vizuri katika kuhakikisha Wananchi na waumini wa dini ya kiisilamu wanasherehekea sikukuu ya Eid katika hali ya utulivu na amani.
Hayo yamesemwa leo Mei 2,2021 na Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza Ramadhani Ng’anzi wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya namna walivyojipanga kuimarisha ulinzi kwenye sikuku hiyo.
Ng’anzi amesema kuwa Jeshi hilo linatambua kuwa sikukuu watu mbalimbali wanaenda kusherehekea kwenye fukwe za ziwa Viktoria na ndio maana wameimarisha ulinzi kwa kutoa askari wa kutosha kwa lengo la kuimarisha ulinzi.
Amesema kuwa Jeshi hilo pia limetoa askari wa kutosha wa usalama barabarani vikiwemo vifaa mbalimbali vya kupima ulevi,magari ya doria pamoja na pikipiki ambazo zitakuwepo muda wote ili kuweza kuwakagua wale ambao wanavunja sheria za Nchi.
Ng’anzi amewaasa wazazi na walezi kuwa wasiwaruhusu watoto kwenda sehemu za mikusanyiko kwa lengo la kusherehekea wakiwa wenyewe kwani kwakufanya hivyo wataepukana na changamoto ya kupotea kwa watoto.