Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Bw Juma Mkomi akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Mambo ya Kale wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Naibu Katibu Mkuu akizungumza na wakuu wa idara mbalimbali wa Manispaa ya Lindi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa (hawamo pichani) alipowasili mjini Lindi kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya `uviko 19 inayotekelezwa na Makumbusho ya Taifa
Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Bw. Juma Mkomi (mwenye kofia) akikaribishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga (kushoto kwake) na Mkurugenzi wa Maspaa ya Lindi, Juma Ali mara alipowasili Lindi.
**************************
Na Joyce Mkinga, Lindi
Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Bw. Juma Mkomi ameitaka Makumbusho ya Taifa la Tanzania kufanya utafiti zaidi wa vivutio vya malikale katika Mkoa wa Lindi ili yaweze kuhifadhiwa
Bw. Mkomi ameyasema haya mjini hapa wakati wa ukaguzi wa miradi ya malikale ya UVIKO 19 yanayotekelezwa na Makumbusho ya Taifa.
Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa Mkoa wa Lindi una vivutio vingi vya malikale na kimakumbusho hivyo, utafiti zaidi ufanyike ili kubaini vivutio hivyo na kupata taarifa zake ili viweze kuhifadhiwa.
“Lindi ina vivutio vingi vya kimakumbusho, malikale na fukwe nzuri ambavyo vikifanyiwa utafiti na kuwa na taarifa mahsusi vitawavutia watalii wengi wa ndani na wa nje ya nchi,” amesema Bw. Mkomi.
Ameyataja baadhi ya maeneo ambayo ni maarufu lakini hayana taarifa za kutosha ili kuhifadhiwa kuwa ni pamoja na Jiwe la Mzungu, ghofu la Kiswele ambalo ilikuwa hoteli waliopumzika wageni kutoka Kenye na nchi zingine.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu ameitaka Makumbusho ya Taifa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya UVIKO 19 ili iweze kuleta tija kwa Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga alimshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa kutenga muda wa kutembelea miradi hiyo. Aliitaja miradi inayotekelezwa katika mkoa wa Lindi kwamba ni pamoja na ujenzi wa vituo cha taarifa katika eneo la Mikumbi na Mkwajuni, Tendaguru pamoja na ukarabati wa ngome ya kihistoria iliyojengwa katika kipindi cha karne ya 19.
Mingine ni ujenzi wa taswira mbili za mjusi mkubwa (dainasoria) aliyeishi miaka mingi iliyopita katika eneo la Tendaguru. Taswira moja itajengwa katika mzunguko wa Barabara ya Fisi mjini Lindi na nyingine itajengwa eneo la Mkwajuni.
Mradi mwingine ni usimikaji wa vibao elekezi/taarifa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kiranjeranje, Kitumbini, Mnyangala, Mkwajuni, Tendaguru na Lindi Mjini.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, Bw. Juma Ali aliishukuru Serikali kwa miradi iliyoelekezwa katika mkoa wa Lindi na kwamba miradi hiyo ikikamilika itaupo mkoa huo sura mpya ya kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi.