Uongozi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke kwa kushirikiana na Wadau wa Mahakama umeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya shughulikia changamoto ya kuchelewa kwa malipo ya mirathi pindi Msimamizi wa Mirathi anapofuatilia malipo na stahiki mbalimbali za marehemu.
Uamuzi huo ulifikiwa katika Kikao cha wadau kilichofanyika katika Kituo hicho hivi karibuni kilicholenga kushughulikia changamoto za kuchelewa kwa malipo ya mirathi kutokana na sababu mbalimbali.
Wadau walioshiriki katika kikao hicho ni Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya “NSSF na PSSF”, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mamlaka ya Mapato (TRA), Soko la Hisa Dar es Salaam. Wengine ni Taasisi za Kibenki, Kampuni za Simu, pamoja na wadau wanaofanya kazi katika kituo hicho.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa kituo hicho, Mhe. Ilvin Mugeta alisema kuwa lengo la kikosi kazi hicho ni kubainisha mahitaji ya nyaraka yanayohitajika katika Taasisi mbalimbali ili kuondoa usumbufu wa muda na gharama kwa msimamizi na warithi hatimaye kuharakisha warithi kupata haki zao kwa wakati.
“Zipo changamoto za mahitaji yasiyo ya lazima na kisheria yanayowapa wakati mgumu wasimamizi, kwa mfano; Msimamizi wa Mirathi anadaiwa cheti cha Kifo mahakamani anapofungua shauri la Mirathi. Sheria inataka cheti hicho kibakie hapo hadi atakapokamilisha taratibu za mirathi. Msimamizi huyo huyo wa mirathi atadaiwa cheti hicho (ambacho sasa hana) anapoenda benki na kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Ni muhimu tukubaliane namna bora ya kumhudumia mwananchi huyo’ alisema Jaji Mugeta.
Aidha katika majadiliano wadau mbalimbali walioshiriki katika kikao hicho, walibaini kuwa, ipo haja ya kuona namna gani baadhi ya changamoto zinazoweza kuepukika kwa kutumia mifumo ya TEHAMA inayosomana baina ya Taasisi kuhakiki nyaraka ili kuharakisha upatikanaji wa haki za warithi na kuepusha udanganyifu.
Akitoa neno la shukrani wakati wa kufungwa kwa kikao hicho, Mwakilishi wa PSSF, Bi. Ritha Ngalo alieleza kwamba kikao hicho kimekuwa ni jukwaa muhimu kwa wadau kuwa na uelewa wa pamoja juu ya taratibu za mirathi katika kituo hicho lakini pia namna bora ya kushughulikia taratibu za mafao yanayohusu mirathi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Temeke/Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Ilvin Mugeta (aliyesimama) akitoa hotuba yake kwenye kikao cha Wadau. Kushoto ni Jaji wa Kituo hicho, Mhe. Dkt Modesta Opiyo na kulia ni Kaimu Msajili- Mahakama Kuu, Mhe. Arnold Kirekiano.Mhe. Jaji Ilvin Mugeta (aliyesimama) akiongoza majadiliano ya wajumbe katika kikao.