Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Mei Mosi Taifa 2022, Roselyne Massam (kulia) akimkabidhi boksi la biskuti Sr. Elizaberth Mtema wa kituo cha Nyumba ya Matumaini kilichopo Miyuji ikiwa ni moja ya majitoleo yaliyotolewa na wachezaji walioshiriki kwenye michezo hiyo iliyofanyika jijini Dodoma takribani kwa siku 14.
Mlezi wa Kituo cha Watoto wenye uhitaji cha Miyuji, Sr. Bertha Ligoha (kulia) pamoja na Watoto wakipokea zawadi mbalimbali za vyakula, sabuni na nguo kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Mei Mosi Taifa 2022 (kushoto), Roselyne Massam. Katikati ni mchezaji Joram wa timu ya Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC).
Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Mei Mosi Taifa, Twaibu Dowile akiwa kwenye picha na baadhi ya Watoto wenye uhitaji wa kituo cha Miyuji cha jijini Dodoma, ambapo wanamichezo walioshiriki kwenye mashindano hayo walikwenda kutoa misaada mbalimbali.
Sr. Rosaria Garciuzo wa Kituo cha Watoto wenye uhitaji cha Kijiji cha Matumaini (kushoto) akimpa mkono wa shukrani Makamu Mwenyekiti DSC wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa 2022, Roselyne Massam baada ya kumkabidhi vyakula mbalimbali kwa ajili ya Watoto 155 wenye uhitaji wanaolelewa kwenye kituo hicho. Mahitaji hayo yamenunuliwa na wachezaji Zaidi ya 1,000 waliokuwa wakishiriki Mashindano ua Mei Mosi Taifa 2022 jijini Dodoma.
Baadhi ya wachezaji kutoka timu mbalimbali zilizoshiriki wenye michezo ya Mei Mosi Taifa 2022 wakishiriki kwenye zoezi la kutoa zawadi kwa Watoto wa vituo vya Watoto wenye uhitaji vya jijini Dodoma.
***********************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WANAMICHEZO takribani 1000 waliokuwa wakishiriki kwenye mashindano ya Kombe la Mei Mosi Taifa 2022 yaliyofanyika jijini hapa wamewakumbuka Watoto wenye uhitaji kwa kuwatembelea na kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu.
Wanamichezo hao wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Mei Mosi Taifa 2022, Roselyne Massam amesema wameweza kuchangishana fedha na kununua mchele, maharage, nguo, sabuni, sukari, juisi, biskuti, mafuta ya kujipaka na mafagio; na uniti za umeme wa Tshs 200,000 na kuvigawanya na kuvipeleka kwenye vituo vitatu vya Watoto wenye uhitaji.
Vituo vilivyosaidiwa ni pamoja na Nyumba ya Matumaini iliyopo Miyuji yenye jumla ya Watoto 62; kituo cha pili ni Miyuji chenye Watoto wenye 20 ambao wanasimamiwa na Watawa wa Shirika la Mtakatifu Gemma; na kituo cha tatu ni Kijiji cha Matumaini chenye Watoto 155 wakiwa wa kike ni 85 na wakiume ni 70 wenye rika mbalimbali.
Massam amewashukuru wanamichezo na taasisi zote zilizoguswa na kutoa michango yao iliyofanikisha kununuliwa kwa mahitaji mengi yaliyoweza kugawanywa kwenye vituo hivyo.
“Kwa namna ya pekee mimi binafsi na kwa niaba ya kamati ya michezo tunawapongeza sana wanamichezo waliowiwa na kutoa michango kwa ajili ya Watoto wenye uhitaji, tumeweza kununua vitu vingi vilivyogawanywa kwenye vituo vitatu; pia nawashukuru TANESCO (shirika la Umeme nchini kwa kuweza kutoa umeme wa Tshs 200,000 zilizogawanywa kwa kila kituo ambapo zimegawanywa Tshs 40,000, 80,000 na 80,000,” amesema Massam.
Naye Sr. Elizaberth Mtema, ambaye ni mlezi wa Nyumba ya Matumaini amewashukuru wanamichezo kwa kuwa na moyo wa kutoa na amewaombe kwa Mwenyezi Mungu akawape Zaidi ya walizotoa.
Halikadhalika Sr. Bertha Ligoha wa kituo cha Miyuji, ameshukuru kwa msaada huo kwenye kituo hicho kinachowahudumia Watoto wenye ulemavu wa akili na kina Watoto 20 wakiwa ni sita wa kike na 14 wa kiume.
Kwa upande wake Sr. Rosaria Garciuzo wa kituo cha Kijiji cha Matumaini amewaombea baraka nyingi wanamichezo walioguswa na kutoa misaada kwenye kituo hicho chenye Watoto wengi, na kuomba watu wengine wenye kuwiwa kujitokeza kusaidia Watoto hao ambao bado wanauhitaji wa mahitaji mengi ya kibinadamu.
Pia amewakaribisha wananchi wenye mapenzi mema kushiriki nao tarehe 17 Agosti, 2022 katika misa ya shukrani na sherehe kwa kituo hicho kutimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.