Na Abby Nkungu, Singida
MWAMKO duni wa wazazi kuwachangia chakula cha mchana watoto wao wanaosoma bado ni changamoto kubwa ambapo asilimia 66.1 ya shule za msingi za Serikali katika Manispaa ya Singida hazitoi huduma hiyo.
Hali hiyo inatajwa kuathiri usikivu, umakini, uelewa na ufaulu hasa kwa watoto wasiozidi miaka minane ambao bado wanahitaji lishe bora kwa ajili ya ukuaji wa ubongo ili waweze kufanya vyema darasani.
Ofisa elimu Msingi Manispaa ya Singida, Omary Maje alisema kuwa kati ya shule 53 za msingi za Serikali zilizopo halmashauri hiyo, 18 tu (sawa na asilimia 33.9) ndizo zinazotoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wake.
“Manispaa hii kuna jumla ya shule 71. Shule 53 ni za Serikali, 13 binafsi na 5 za awali tu. Wenzetu wa binafsi shule zote zinatoa chakula cha mchana na uji ndio maana hata ufaulu wao ni mzuri lakini sisi wa Serikali ni shule 18 tu ndizo zenye huduma hiyo” alifafanua Maje.
Alisema kuwa tatizo kubwa ni mwamko mdogo wa wazazi na walezi kushindwa kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao shuleni lakini akasisitiza kuwa idara hiyo inaendelea na juhudi za kuwapa wazazi hao ujumbe sahihi na kuwaeleza manufaa yake; ikiwa ni pamoja na kuwaongezea usikivu, umakini na uelewa kwenye masomo yao.
“Hata hivyo, tunashukuru kwani kuna ongezeko kubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa Oktoba mwaka jana ambapo ni shule nne tu za Serikali ndizo zilizokuwa zinatoa chakula. Baada ya kubanana na nyie vyombo vya habari kuandika-andika, hatimaye leo tumefikia shule 18 zenye huduma hiyo, sio jambo dogo” alieleza.
Alisema kuwa Manispaa ya Singida ni miongoni mwa halmashauri nchini zinazotekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya miaka mitano (2021 – 2026 ) ambapo suala la lishe mashuleni na hasa kwa watoto walio chini ya miaka minane linapewa kipaumbele.
Mmoja wa walimu wanaofundisha shule ya awali ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema ni vyema juhudi hizo zikaharakishwa ili watoto wapate elimu bila kikwazo chochote.
“Wanaoumia zaidi na changamoto hii ni hawa watoto wadogo ingawa baadhi yao huwahi kuondoka shule lakini kwa wanaobaki ikifika saa 4:00 asubuhi huwa wanaanza kusinzia na kupiga miayo kwa njaa na uchovu hadi unawahurumia, wanapoteza usikivu kabisa” alisema.
Halima Omari, mzazi na mkazi wa Majengo na John Lameck mkazi wa Ginnery Manispaa ya Singida, pamoja na kukiri juu ya adha ya njaa hasa kwa watoto wa chekechea na madarasa ya chini, wanawatupia lawama viongozi na watendaji wa Serikali wakidai wameshindwa kuhamasisha vya kutosha suala hilo.
“Mbona michango mingine tunatoa…..ujenzi wa madarasa, maabara, vyoo, Mbio za Mwenge, harusi na kipaimara. Iweje chakula tena cha mtoto wangu mwenyewe nisichangie? Tatizo ni viongozi wetu” alisema John huku akiungwa mkono na Halima ambaye ametaka viongozi na watendaji kutimiza kikamilifu wajibu wao.
Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, ulaji duni au ulaji usiozingatia makundi matano ya chakula huathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto hivyo kusababisha kutokufundishika kirahisi darasani na kuwa mzito kwenye kufikiri na kutoa uamuzi sahihi anapokuwa mtu mzima.