Wachezaji Bestina Kazinja wa Wizara ya Mambo ya Ndani akidaka mpira kutoka kwa Mariam Shabaan (hayupo pichani), huku Mary Kajigiri wa Uchukuzi SC akinyoosha mikono kuzuia mpira huo katika mchezo wa fainali wa Kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa. Mambo ya ndani wametwaa ubingwa kwa kushinda kwa magoli 50-34.
Kiungo Hafidh Mohamed wa timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (kulia) akipiga shuti langoni mwa timu ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) huku kipa Leonard Mkinga akijaribu kuokoa hatari hiyo. Maliasili wameibuka mabingwa wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa iliyomalizika hivi karibuni kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa kwa kushinda kwa mikwaju ya penati 4-3.
Mwenyekiti wa Uchukuzi SC (mwenye miwani) akipokea kombe la ushindi wa ujumla wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa kutoka kwa mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Serikali Kuu na Afya, (TUGHE), Dkt Jenny Ndeta kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Kikosi cha Idara ya Mahakama (kushoto) kikiburuzwa na wenzao wa Uchukuzi katika mchezo wa fainali wa kuvuta kamba wanaume wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Uchukuzi wametwaa ubingwa kwa mivuto 2-0.
Mmoja wa makocha wa mchezo wa kuvuta kamba wa timu ya Uchukuzi SC, Nicas Luvanda akibebwa juu juu na wachezaji wa timu wakifurahia baada ya klabu hiyo kutwaa ubingwa kwa wanaume na wanaume katika michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa iliyofanyika jijini Dodoma.
Nahodha Bahati Herman wa mchezo wa netiboli wa timu ya Uchukuzi SC akipokea kombe la mshindi wa pili wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa kutoka kwa mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Serikali Kuu na Afya, (TUGHE), Dkt Jenny Ndeta kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma. Uchukuzi walifungwa na Mambo ya Ndani kwa magoli 50-34 katika mchezo wa fainali.
Wachezaji wa timu ya Uchukuzi wanawake (kushoto) wakiwavuta timu ya Idara ya Mahakama na kutwaa ubingwa wa michuani ya Kombe la Mei Mosi Taifa iliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwa mivuto 2-1 baada ya mivuto ya kawaida kutoka sare ya 1-1.
……………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire ameitaka klabu ya michezo ya sekta hiyo, Uchukuzi SC kujenga tabia ya kukuza vipaji vipya vitakavyoleta ushindani kwenye mashindano mbalimbali yanayohusisha watumishi wa umma na binafsi, kwa kuwa vitasaidia kuokoa jahazi endapo waliokuwepo sasa watapata matatizo ya kibinadamu.
Akitoa kauli hiyo katika hafla ya kuipongeza timu hiyo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Sekta hiyo, Lucas Kambelenja aliyemwakilisha Katibu Mkuu amesema vipaji vipya vitaleta ushindani mkubwa na kuongeza chachu ya ushindi kwa klabu hii.
“Hata maofisini kuna mfumo wa kurithishana endapo mzoefu au mbobezi hayupo mwingine mwenye kada husika anaweza kufanya vyema bila tatizo, hivyo ninaimani kubwa tukifanya hivi katika timu yetu tutaongeza ubingwa kwenye michezo yote tutakayoshiriki,” amesema Kambelenje.
Hatahivyo, ameipongeza klabu ya michezo ya Uchukuzi SC kutwaa ushindi wa jumla kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuzoa vikombe sita vya ushindi wa michezo ya mbalimbali iliyoshindaniwa kwenye michuano ya Mei Mosi Taifa iliyokuwa ikifanyika jijini hapa. Mwaka 2021 walipata ushindi wa jumla kwa kuzoa vikombe 13 michuano hiyo ilifanyika Jijini Mwanza.
“Wizara inawapongeza sana na tutaendelea kuwa nanyi bega kwa bega kwa kuwa mmeendelea kututangaza na kutuheshimisha kupitia michezo, tunawapongeza sana kwa bidii na jitihada mlizoonesha kipindi chote cha mashindano hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa wa jumla tena ikiwa ni kwa mwaka wa pili mfululizo, na ninazipongeza taasisi zote 13 zilizotoa washiriki wa michezo hii,” amesema Kambelenja.
Halikadhalika amewakumbusha viongozi wa klabu hiyo kupanga programu endelevu ya mazoezi na mabonanza kwa mtindo wa kutoka taasisi moja na kwenda nyingine, ili kuendelea kuiweka sawa miili ya wafanyakazi tayari kwa kushiriki kwenye mashindano mbalimbali yakiwemo ya Shirikisho la michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) itakayofanyika baadaye mwaka huu, na hata kujenga afya zao ili kuongeza ufanisi wa kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu hiyo, Andrew Magombana amesema klabu hiyo imepata mafanikio makubwa kwa kutwaa ubingwa wa jumla baada ya kupata vikombe vya ushindi wa kwanza katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume na wanawake; mabingwa wa mbio za baiskeli kwa wanawake; pia wameshika nafasi ya pili katika mchezo wa netiboli na ushindi wa tatu wa baiskeli wanaume na ushindi wa tatu wa jumla katika mchezo wa riadha baada ya kujisanyia alama 29.
Katika michezo hiyo iliyoanza April 16 na kufikia tamati April 29, 2022 Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wametwaa ubingwa wa mchezo wa draft kwa wanawake, huku Halmashauri ya Kongwa wakitwaa kwa upande wa wanaume; nao Taasisi ya Saratani Ocean Road wameibuka mabingwa katika mchezo wa bao kwa wanaume, na Wizara ya Mambo ya Ndani wametwaa kwa wanawake; halikadhalika ushindi wa kwanza wa riadha umechukuliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Timu nyingine zilizotwaa ubingwa ni Wizara ya Mambo ya Ndani imetwaa ubingwa wa mchezo wa netiboli, wakati Wizara ya Maliasili na Utalii umetwaa ubingwa wa soka, nao Taasisi ya Saratani Ocean Road wametwa ubingwa wa mbio za baiskeli kwa wanaume; wakati Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wametwaa ubingwa wa mchezo wa karata kwa wanawake, huku kwa wanaume ubingwa ukienda kwa Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC).
MWISHO