Mwandishi
wetu – DODOMA
Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umepata tuzo tatu katika kilele cha Maadhimisho
ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ambapo kwa Tanzania yamefanyika
katika viwanja vya Kituo cha Mikutano Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Akizungumza
wakati wa kilele hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka waajiri na
wafanyakazi kuendelea kushirikiana pamoja ili kuweka mzingira yenye usalama na
afya katika maeneo ya kazi ikiwemo kuzuia vihatarishi.
Amefafanua
kuwa, kuweka mazingira salama kunapunguza gharama kwa sababu wafanyakazi
wanapopata ajali au ugonjwa kutokana na kazi inavuruga mipango ya uzalishaji
kwa pande zote mbili.
“Waajiri
na wafanyakazi ni lazima wafahamu suala la afya na usalama mahali pa kazi ni
mkakati wa pamoja na ni sehemu ya utekelezaji wa Mfumo wa haki na wajibu
ulioainishwa kimataifa na kanuni ya kuzuia vihatarishi inapewa kipaumbele cha
juu zaidi”, alieleza Waziri Ndalichako.
Wakati
huohuo, Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeahidi kushirikiana na Serikali ya Rais
Samia Suluhu Hassan kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili kuongeza
ufanisi wa kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua au
kufariki kutokana na kazi.
Ahadi
hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Shirika hilo, Ndg. Getrude Sima baada ya WCF
kushinda tuzo tatu katika maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi
Duniani ambapo kwa Tanzania yamefanyika katika viwanja vya Kituo cha Mikutano
Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
“Tutaendelea
kushirikiana na WCF kupitia mikakati yetu mbalimbali ndani ya Shirika la Kazi Duniani
hapa Tanzania kwa hiyo niwapongeze sana na nimefurahi kuona kwamba nanyi pia
mmeweza kushiriki na kuwaeleza wananchi mnachofanya,” ameeleza Ndg. Sima.
Naye
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hery
Mkunda ameipongeza WCF kwa kushinda tuzo nyingi zaidi na kuitaka Taasisi hii
kuendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.
Akizungumzia
maadhimisho haya, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema Mfuko huu umekwisha
lipa fidia kwa wafanyakazi mbalimbali waliopata ajali wakiwa kazini na baadhi
yao wameshiriki katika Maadhimisho haya.
Kuhusu
huduma zilizotolewa amesema WCF imeshirikisha wanufaika wao katika kutoa elimu
ya fidia kwa wadau waliotembelea Maadhimisho haya. Pia imeweza kuonesha viungo
bandia vinavyolipiwa na WCF kwa wahitaji wa viungo hivyo, pamoja na uwepo wa
madaktari tunaoshirikiana nao katika utoaji wa huduma mbalimbali za kitabibu”, amehabarisha
Dkt. Omar.
Sambamba
na hayo, wanufaika wa Mfuko huo, wameishukuru Serikali kwa kuanzisha WCF ambayo
imeweza kuwalipia gharama za matibabu, kuwanunulia viungo bandia ikiwemo miguu
na mikono bandia pamoja na kuwalipa pensheni kila mwezi huduma ambayo
itaendelea mpaka mwisho wa uhai wao.
“Mbali
na pensheni ninayopata kila mwezi, WCF walinililipa fidia ambayo imeniwezesha
kununua bajaji na nimejiajiri kama dereva. Nashukuru sana kwani naihudumia
familia yangu kama nilivyokuwa kabla ya ajali,” amearifu Ndg. Deus Anthony.
Naye Bw. Hamisi Omari ameshukuru kwa kutibiwa, kununuliwa mkono wa bandia na kuendelea
kulipwa pensheni kila mwezi.
Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi umepata tuzo ya Mwajiri Bora katika Sekta za Bima,
Hifadhi ya Jamii na Usalama Mahala pa Kazi, tuzo ya Muoneshaji Bora katika
kujali Wafanyakazi wenye Mahitaji Maalum na tuzo ya Mshindi wa tatu katika
Taratibu za Usimamizi wa Usalama Mahala pa Kazi kwa Sekta ya Umma.
WCF
ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoanzishwa kwa lengo la kushughulikia masuala
ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara
ambao wanaumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako(kushoto), akimkabidhi Meneja Tathmini za Vihatarishi Sehemu za Kazi kutoka WCF, Bi. Naanjela Msangi, Moja ya tuzo hizo