Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka,akizungumza wakati wa kikao kazi cha watunza kumbukumbu na nyaraka za serikali chenye lengo la kujadili masuala ya utunzaji wa kumbukumbu katika utumishi wa umma jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa TRAMPA Francis Zengo Mathias akizungumza katika kikao kazi cha watunza kumbukumbu na nyaraka za serikali chenye lengo la kujadili masuala ya utunzaji wa kumbukumbu katika utumishi wa umma jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watunza kumbukumbu na nyaraka za serikali jijini Dodoma.
…………………………………………
Na Bolgas Odilo, Dodoma.
Watunza kumbukumbu na nyaraka za serikali wametakiwa kuhakikisha kumbukumbu na nyaraka zinatunzwa vizuri kwa kuzingatia uadilifu, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na Serikali ili kurahisisha utendaji kazi wao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka wakati wa kikao kazi cha watunza kumbukumbu na nyaraka za serikali chenye lengo la kujadili masuala ya utunzaji wa kumbukumbu katika utumishi wa umma jijini Dodoma.
Mtaka amesema, uadilifu katika kutekeleza majukumu yetu ni jambo la msingi sana hivyo kwa wale ambao si waadilifu wabadilike ili tuweze kuwa na mchango katika kujenga utumishi wa umma uliotukuka.
“Watunza nyaraka wote wa ofisi na taasisi za kiserikali kuweni waadilifu na mfuate kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa katika utendaji wenu wa kazi katika taasisi mlizopo.
“Najua kuna changamoto nyingi mnakutana nazo maofisini kwenu na nyingine mmezitaja hapa, hivyo basi msiache kuwa waadilifu hata kama viongozi wenu watakuwa hawawathamini,” alisema Mtaka.
Sanjari na hayo, Mtaka amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kufanya masijala ni kama sehemu ya kuwaweka watu kutumikia adhabu wanazopewa endapo wakifanya makosa.
“Masijala sio sehemu ya mtu kutumikia adhabu kwa mtumishi wa juu aliyefanya kosa, haiwezekani kumpeleka mtu ambaye hana taaluma ya utunzaji kumbukumbu akafanye kazi ya kutunza kumbukumbu,” alisema Mtaka.
Naye Katibu Mkuu wa TRAMPA Francis Zengo Mathias ameahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika taasisi za umma uwe na manufaa katika utendaji kazi wa taasisi na kwa maendeleo ya taifa.