Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifunga kongamano la kwanza la ufuatiliaji na tathmini nchini lililofanyika jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wa kongamano la ufuatiliaji na tathmini wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akifunga kongamano la kwanza la ufuatiliaji na tathmini nchini lililofanyika jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Hassan Kitenge akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga kongamano la kwanza la ufuatiliaji na tathmini nchini lililofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Udara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi, Bw. Nolasco Kipanda akiwasilisha kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi maazimio ya kongamano la kwanza la ufuatiliaji na tathmini nchini wakati Naibu Waziri huyo alipokuwa akifunga kongamano hili jijini Dodoma.
…………………………………………..
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewasisitiza watendaji katika taasisi za Serikali kuzingatia maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ya kuimarisha eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuwa na mipango yenye tija kwa maendeleo ya taifa.
Akifunga kongamano la kwanza la ufuatiliaji na tathmini nchini lililofanyika katika ukumbi wa PSSSF (Makole) jijini Dodoma, Mhe. Ndejembi amesema Mhe. Waziri Mkuu katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano hilo alitoa maelekezo ya namna ya kuboresha masuala ya ufuatiliaji na tathmini pamoja na kongamano kwa miaka ijayo ili kubaini nchi imepiga hatua kwa kiasi gani katika maendeleo, inakabiliana na changamoto zipi kufikia malengo na hatua za kuchukua kukabiliana na changamoto hizo.
Mhe. Ndejembi amesema kongamano hilo lililenga kuwakutanisha watalaam na watendaji wa ufuatiliaji na tathmini wa ndani na nje ya nchi ili kujadili masuala ya ufuatiliaji na tathmini.
“Nina imani kuwa kupitia kongamano hili, mmepata fursa ya kubadilishana uzoezi na kuongeza uelewa kwenye masuala ya ufuatiliaji na tathmini, uzoefu mlioupata uwe ni chachu katika kuboresha namna ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya ufuatiliaji na tathmini katika taasisi zetu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amezipongeza taasisi zote zilizopata tuzo na kutaka tuzo hizo ziwe chachu ya kuongeza uwajibikaji na kuzitaka taasisi nyingine za Serikali kufanya vizuri kwenye eneo la ufuatiliaji na tathmini sio kwa ajili ya kupata tuzo tu bali kuimarisha utendaji kazi katika taasisi zao.
Kongamano hilo la kitaifa lililofanyika kwa mara ya kwanza nchini liliwashirikisha watalaam wa masuala ya ufuatiliaji na tathmini kutoka nchi mbalimbali ambazo ni Tanzania, Marekani, Uingereza, Ghana, Afrika ya kusini, Kenya, Uganda na Zimbabwe.