***********************
* Asema Serikali itahakikisha uhuru wa vyombo vya habari unaimarishwa na kulindwa
HABARI ni moja kati ya haki za msingi za binadamu kwa kuwa kila mwananchi anayo haki ya kupokea au kutoa habari kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Vyombo vya habari vimepewa jukumu la kutoa habari, kuburudisha na kuelimisha jamii kuhusu matukio na masuala mbalimbali yanayojitokeza ndani na nje ya nchi. Upatikanaji wa habari sahihi na kwa wakati huchangia katika kukuza uchumi, kuimarisha demokrasia na utawala bora.
Hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua vituo vya Kurushia Matangazo ya Redio vya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Wilayani Ruangwa – Lindi kwa niaba ya vituo vingine vya wilaya za Ludewa (Njombe), Mlimba (Morogoro) na Ngara (Kagera).
“Tukio la leo pamoja na kuzinduliwa kwa matangazo ya redio katika vituo vya Ruangwa, Ludewa, Kilombero (Mlimba), Ngara na maeneo ya jirani ni utekelezaji wa ahadi za CCM kwa wananchi kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025.”
Waziri Mkuu alisema Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2020/2021 – 2025/2026) umeainisha vipaumbele vyake katika uwekezaji wa miundombinu ya utangazaji ya TBC, ikiwemo upanuzi wa usikivu wa redio, pamoja na miundombinu.
“Kadhalika, Ilani ya Uchaguzi ya CCM (Ibara 125) inaielekeza Serikali kuwekeza katika uimarishaji wa miundombinu ya utangazaji kwa TBC. Hivyo, kuzinduliwa kwa matangazo ya Redio katika vituo vya Ruangwa, Ludewa, Kilombero (Mlimba), Ngara na maeneo ya jirani ni utekelezaji wa ahadi za CCM kwa wananchi kwa kipindi cha 2020 hadi 2025.”
Aidha, Waziri Mkuu aliwapongezea watendaji wa wizara na taasisi zilizo chini yake kwa kutekeleza kwa vitendo mpango huu wa Taifa kwa wananchi wa Wilaya ya Ruangwa, Ludewa, Kilombero (Mlimba), Ngara na maeneo ya jirani.
Alisema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inajenga miradi hiyo ikiwa ni hatua muhimu katika kutekeleza malengo yake ya kufikisha habari kwa wananchi wote na mahala popote.
“Nia ya Serikali ni kuendelea kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha umma kwa njia ya redio, televisheni na mitandao ya kijamii. Nitumie fursa hii kuwapongeza TBC na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) kwa kazi nzuri.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema katika kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi vyombo vya habari havina budi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi pamoja na kutanguliza uzalendo na maslahi ya Taifa.
Pia, alisisitiza kwamba Serikali itaendelea kusimamia matumizi ya mitandao ya kijamii ili pamoja na kuongeza upatikanaji wa habari kuwepo na uzingatiaji wa maadili na weledi. “Ni matarajio yetu kuwa moja ya majukumu yenu ni kulisemea Taifa letu.”
Alisema Serikali itahakikisha uhuru wa vyombo vya habari nchini unaimarishwa na kulindwa na akawataka wamiliki na wanahabari wanatakiwa wazingatie maadili na weledi katika kazi zao ili wananchi waendelee kupata taarifa sahihi kwa urahisi zaidi na kwa wakati.
Alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wamiliki wa vyombo vya habari wahakikishe wanahabari wanapatiwa mikataba ya ajira inayozingatia sheria za ajira sambamba na kufanya utafiti wa habari ili kuepuka upotoshaji kwa kuchapisha au kutangaza taarifa zinazolenga kuchonganisha jamii.
Pia, Waziri Mkuu aliielekeza TBC, UCSAF na TANESCO kukaa pamoja na kuhakikisha wanatatua changamoto zikiwemo za kukatika katika kwa umeme zinazokabili baadhi ya vituo kama vile Ludewa, Mbinga na Kisaki kwa lengo la kuwapatia wananchi wetu huduma ya Habari na Mawasiliano. “.”
“Ninatambua kuwa Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya TBC ili kutatua changamoto za usikivu. TBC inatekeleza miradi ya upanuzi wa usikivu kwa fedha za Miradi ya Maendeleo katika wilaya za Karagwe (Kagera), Same (Kilimanjaro), Sikonge (Tabora), Kahama (Shinyanga), Bunda (Mara), Nkasi (Rukwa), Kasulu (Kigoma), Kilwa (Lindi), Serengeti (Mara).”
Miradi mingine inatekelezwa katika mikoa ya Njombe, Simiyu na Songwe pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba upande wa Tanzania Zanzibar. Alisema kukamilika kwa miradi hii kutawezesha usikivu wa TBC kufikia Wilaya 120 sawa na asilimia 83 kutoka wilaya 103 sawa na asilimia 64 za usikivu wa sasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema mradi wa ujenzi wa kituo hicho umegharimu shilingi milioni 430 kwa udhamini wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Pia vituo vingine vitatu vilivyozinduliwa leo navyo ujenzi wake umedhaminiwa na UCSAF.
Alisema maeneo mengine ambayo miradi inaendelea kutekelezwa kwa ushirikiano wa TBC na UCSAF ni katika wilaya za Ngara (Kagera), Kyela (Mbeya), Ruangwa (Lindi), Kilombero/Mlimba (Morogoro), Ludewa (Njombe), Mlele (Katavi), Makete (Njombe), Uvinza (Kigoma), Mbinga (Ruvuma) na Ngorongoro (Arusha).
“Ninapenda niwahakikishie kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakusudia kupanua usikivu wa redio za TBC nchi nzima.”
Naye, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashimba alisema mfuko huo utaendelea kushirikiana na Serikali ili kuboresha mawasiliano na usikivu wa huduma za radio kwa kuwafikia wananchi kote nchini.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayoub Ryoba amesema, Shirika hilo limejipanga kuhakikisha wanaendelea kuuhabarisha umma wa wa Tanzania kwa uhakika na weledi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya shirika hilo.