Na Bolgas Odilo_DODOMA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Dodoma imebaini upotevu wa mapato katika Halmashauri ya Mpwapwa kutokana na kuwepo kwa utiriri wa leseni za uchimbaji madini ujenzi.
Takukuru imesema leseni za wachimbaji madini zilizopo ni 773 lakini zinazotumika ni 57 pekee.
Hayo yamesemwa leo April 29,2022 jijini Dodoma na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw.Sosthenes Kibwengo,amesema,taasisi hiyo imefanya chambuzi sita za mifumo katika sekta za mapato ,elimu na ujenzi ambapo imebaini kuwepo kwa utiriri huo wa leseni za uchimbaji madini ujenzi.
Kwa mujibu wa Kibwengo halmashauri zinapoteza mapato katika maeneo ambayo uchimbaji unafanyika kiholela na ambayo hayana mashine za kielektroniki za kukusanya ushuru (POS).
Aidha Kibwengo amesema Mkoa wa Dodoma umefuatilia utekelezaji wa miradi 41 yenye thamani ya shilingi bilioni 11.2 katika sekta za maji,ujenzi,elimu na afya ambapo inajumuisha na miradi ya mpango wa maendeleo wa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19.
Amesema katika eneo hilo miradi 10 sawa na asilimia 24 ilikutwa na mapungufu madogo kama ya kuchelewa kukamilishwa kwa mujibu wa mkataba jambo lililosababisha kuongezeka kwa gharama ,matumizi ya vifaa visivyokidhi ubora na manunuzi kwa gharama ya bei ya soko.
Aidha, amesema mradi mmoja ulikuwa na viashria jinai na hivyo uchunguzi umeanzishwa huku akisema shilingi milioni 409.4 zilizolipwa kwa mkandarasi kinyume na taratibu katika utekelezaji wa mradi mmoja zilirejeshwa kwa kushirikiana na halmashauri husika.
Pia,amesema Takukuru imebaini kuwa kuna ufahamu mdogo kwa kamati za shule kuhusu matumizi ya mfumo wa manunuzi wa ‘force account’
Kuhusu uchambuzi wa mfumo wa viashiria vya rushwa ya ngono katika sekta ya Elimu ngazi ya Halmashauri ,imebainika kuwa maeneo hatarishi kwa uwepo wa rushwa ya ngono ni katika upangaji wa vituo vya kazi kwa asilimia 72 na uhamisho ndani ya halmashauri kwa asilimia 63.
Kwa mujibu wa Kibwengo ,katika kipindi cha robo ya Januari hadi Machi mwaka huu ,taasisi hiyo imepokea malalamiko 133 ambapo taarifa za rushwa zilikuwa ni 66 na zisizo za rushwa ni 67.
Amesema,taarifa 66 kuhusu rushwa zilikuwa katika sekta tisa ambapo Sekta ya serikali za Mitaa ilionyesha kuongoza kwa vitendo hivyo kwa asilimia 19,elimu asilimia 10,Afya asilimia 9,polisi asilimia 5,Mahakama asilimia 4,ardhi aslimia 4 na sekta binafsi asilimia 4 huku taarifa 11 zikihusu watu binafsi.
“Taarifa hizo 66 zinazohusu rushwa zimeshughulikiwa kwa mbinu mbalimbali kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambapo uchunguzi wa majalada 16 ulikamilika na mashauri mapya manane yalifunguliwa na kufanya jumla ya mashauri yanayoendelea mahakamani kufikia 58.”amesema Kibwengo.