Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akikagua nguzo yenye jina la barabara ya Mkoani na Mtaa wa Tanroad wakati wa ziara ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi katika Mkoa wa Manyara.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akikagua kibao cha namba ya nyumba kwenye duka la vifaa vya ujenzi katika Mji wa Babati, wakati wa ziara ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi katika Mkoa huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akikagua vibao vya namba za nyumba wakati vinavyotengenezwa katika Karakana ya Chuo cha VETA Mkoa wa Manyara
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akikagua kibao cha Anwani ya Chuo cha VETA mkoa wa Manyara.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla, akisain kitabu cha wageni alipotembelea karakana ya Chuo cha VETA mkoani Manyara katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi katika mkoa huo.
…………………………………………..
Faraja Mpina na Chedaiwe Msuya, WHMTH, MANYARA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla ametoa rai kwa watendaji wa mkoa wa Manyara kutumia mbinu mbadala katika uwekaji wa miundombinu ya mfumo wa Anwani za Makazi ili kukamilisha zoezi kwa muda uliopangwa na Serikali kwa lengo la kurahisisha zoezi la sensa ya watu na makazi
Abdulla amebainisha hayo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapo kwa ajili ya kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa zoezi la Anwani za Makazi ambapo mkoa wa Manyara upo katika orodha ya mikoa ambayo imetekeleza kwa asilimia chache uwekaji wa nguzo za barabara na mitaa pamoja na namba za nyumba.
Amesema kuwa, “Inawezekana mkaanza kwa kuweka hata nguzo za mbao na kutumia rangi kuchora namba za nyumba ili tukamilishe zoezi hili kwa wakati kwa kuwa zoezi la sensa linategemea miundombinu ya mfumo wa Anwani za Makazi.”
Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka watendaji wa halmashauri zote za mkoa huo kuwa wabunifu na kukamilisha zoezi hilo kwa wakati mahususi kwa ajili ya kurahisha ufanyikaji wa zoezi la sensa na baadae kuboresha zaidi kwa mujibu wa miongozo ya uwekaji wa miundombinu hiyo kupitia mapato yao ya ndani ya halmashauri pamoja na kuhusisha wadau wa maendeleo.
aarifa ya utekelezaji ya mkoa wa Manyara yenye jumla ya halmashauri saba ambazo ni halmashauri mbili za Miji (Babati, Mbulu) na halmashauri tano za Wilaya (Babati, Mbulu,Kiteto, Hanang, Simanjiro) inaonyesha Anwani za Makazi 372,455 zimekusanywa ikiwa ni asilimia 103 ya lengo la kukusanya Anwani 362,987
Aidha, kwa upande wa uwekaji wa miundombinu ya nguzo za barabara na mitaa pamoja na uwekaji wa namba za nyumba linaendelea kufanyika kupitia mapato ya ndani na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za TARURA, TANROAD na VETA za mkoani hapo
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa muda hadi Mei 5, mwaka huu, kwa Mkoa wa Manyara kukamilisha zoezi la uwekaji wa miundombinu hiyo ambapo Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bi. Karolina Mthapula pamoja na watendaji wa halmashauri za mkoa huo waliridhia na kumhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa watajipanga kwa kutumia mbinu mbadala walizopewa na kwa kushirikiana na wadau zoezi litakamilika kwa muda uliopangwa.