Wawasilishaji mada, Bw. Kabeba Maiga (kulia) kutoka St. Justin Centre for Children with Disabilities pamoja na mwenzake Marco Masumbuko kutoka Chuo cha Lake Victoria Disability Center. |
Sehemu ya wadau wa elimu wakifuatilia mada anuai kwenye Kongamano la Elimu lilikutanisha wadau wa elimu nchini kujadili masuala ya elimu jumuishi, Wilaya ya Igunga. |
Bi. Abella Bakalemwa kutoka Shirika la CBIDO la Kagera akiwasilisha mada kwenye kongamano la elimu. |
Afisa Elimu Mkoa wa Tabora, Juma Japhet Kaponda akizungumza kwenye kongamano la elimu. |
Baadhi ya wadau wa elimu wakiwa kwenye Kongamano la Elimu lilikutanisha wadau wa elimu nchini kujadili masuala ya elimu jumuishi, Wilaya ya Igunga. |
Baadhi ya wadau wa elimu wakichangia mada kwenye Kongamano la Elimu lilikutanisha wadau wa elimu nchini kujadili masuala ya elimu jumuishi, Wilaya ya Igunga. |
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batilda Buriani amezinduwa Kongamano la Elimu lilikutanisha wadau wa elimu kujadili masuala ya elimu jumuishi, iliyoanza kutekelezwa na baadhi ya wadau kupitia asasi zao mafanikio na changamoto zake.
Akizungumza kabla ya kuzinduwa kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa aliwataka wadau wa elimu kujadili kwa mawanda mapana suala zima la elimu jumuishi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha suala la elimu jumuishi liende pamoja na ubora na stahiki.
“Tuangalie masuala ya elimu jumuishi yanazingatia pia ubora na stahiki, binafsi naongezea tusitake tu elimu jumuishi ila tuzingatie inakuwa bora na stahiki ili watoto wote waweze kuipata kiusawa bila ubaguzi kuanzia ngazi ya awali, msingi na hadi vyuoni,” alisema Balozi Dk. Buriani.
Alisema Mkoa wa Tabora umeanza vizuri katika kuhamasisha wananchi kuhakikisha wanakuwa sehemu ya mabadiliko na kuondoa vikwazo vya elimu vilivyokuwa vikiuweka mkoa huo kwenye sifa mbaya kielimu, na kwa kuanzia tayari wanajenga mabweni ya wanafunzi wenye ulemavu anuai kusaidia suala zima la upatikanaji usawa kwenye elimu.
“…Taifa lolote litajengwa na kuimarika likiwa na watu wenye ustawi mzuri wa elimu bora, afya, maadili, hofu ya Mungu na uzalendo, ndio maana nasema ipo sababu ya wadau wote wa elimu kushirikiana kukuangalia suala la udhibiti ubora wa elimu,”
Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna changamoto katika suala zima la maadili, ulinzi wa watoto awapo shuleni jambo ambalo haliwezi kufanikiswa na Serikali peke yake, lakini kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu pamoja na jamii kwa ujumla.
“Mara kadhaa yanatokea matukio ya unyanyasaji watoto shuleni, sehemu zingine vitendo vinafanywa na watoto wenzao na pengine walezi wenyewe wa watoto mashuleni, naomba tushirikiane kuliangalia hili kwa pamoja ili kuhakikisha watoto wetu wanakuwa salama, kuanzia wanaoanza shule za awali na hadi ngazi za vyuoni.”
Awali akizungumza katika Kongamano hilo, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga alibainisha kuwa Tanzania iko katika wakati muhimu sana ambao unahitaji dhamira ya dhati kutoka kwa washirika na wadau wote ili kuhakikisha utoaji wa elimu bora bila malipo kwa wote unapatikana kwa wakati kama ilivyoainishwa katika ajenda ya dunia ya Elimu 2030.
“Tunapoendelea kuelekea 2030, tumebakiwa na miaka 8 kufikia lengo namba nne la Elimu (SDG4). Tunaweza kufanikiwa kufikia lengo hili endapo tutashirikiana kwa pamoja duniani kote ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazo kwamisha juhudi zetu,”.