***************************
Na. A/INSP Frank Lukwaro
Jamii imetakiwa kutumia vyema mila ya Jando na Unyago ili iweze kuwasaidia Vijana kujitambua na kuwaelekeza katika kutafuta maendeleo ya maisha yao badala ya kutoa mafunzo ambayo yana lengo la kuwaingiza katika matendo hatarishi ikiwemo kushiriki tendo la ndoa katika umri mdogo.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ya Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Faidha Suleiman wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa madawati ya jinsia na watoto katika Wilaya za Tandahimba, Newala na Nanyumbu Mkoani Mtwara ambapo ameweza kukutana na makundi mbalimbali yanayofanya kazi na Dawati la Jinsia na Watoto ndani ya Jeshi la Polisi.
ACP Faidha amesema mila na desturi hazikatazwi ila zinatakiwa kutumika vyema ili kuleta maendeleo kwa washiriki ikiwemo kuwajengea uelewa washiriki jinsi ya kujikinga na vitendo vya jinai ambavyo vinaweza kuwakuta katika umri mdogo kutokana na baadhi ya mafunzo wanayopata wakiwa katika Jando na Unyago.
Amesema kwakuliona hilo Dawati la Jinsia na Watoto ndani ya Jeshi la Polisi limejikita kutoa elimu kupitia kwa Viongozi wa kimila, Makungwi na Viongozi wa Serikali ili waweze kufikisha kwa urahisi elimu hiyo katika jamii na washiriki wa mila hizo.
Naye Sheikh wa Wilaya ya Nanyumbu Sheikh Yasini Chilombo akizungumza kwa niaba ya Viongozi wa dini amesema watatoa fursa kwa Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto ili waweze kutoa elimu katika misikiti kwa lengo la kufanya jamii kuepukana na vitendo vya ukatili ambavyo vinatokea katika jamii.
Kwa upande wake Kwa upande wake Kiongozi wa Kijamii maarufu kama Chifu katika Wilaya ya Nanyumbu Rashid Mrope amesema Wataanza kujikita katika kutoa elimu ili iweze kuwafikia watu wengi Zaidi na kujikita katika kutoa mafundisho ambayo yatawajenga vijana kujitambua na kuweka muda maalumu wa kufanya mila hizo ili kutoa fursa kwa vijana kupata elimu.