Mratibu wa Tiba asili na Tiba mbadala wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole akikabidhi cheti cha usajili wa tiba asili kwa Mganga wa Tiba asili na tiba mbadala Rabia Rashid.
Mganga wa Tiba asili na tiba mbadala Rozina Mohamed kulia,akipokea cheti cha usajili kwa ajili ya kufanya kazi za tiba asili kutoka kwa Mratibu wa Tiba asili na tiba mbadala wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyeti kwa waganga zaidi ya 37 wanaofanya kazi zao katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Mratibu wa Tiba asili na tiba Mbadala wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole wa tatu kulia akiwa na baadhi ya Waganga wa tiba asili na tiba mbadala baada ya kukabidhi vyeti vya usajili kwa waganga hao.
Picha na Muhidin Amri
………………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Tunduru
WAGANGA wa tiba asili na tiba mbadala na wazalishaji wa Dawa za asili wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wametakiwa kuzingatia ubora wa dawa na huduma wanazotoa ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata wateja wao.
Wito huo umetolewa jana na Mratibu wa Tiba asili na tiba mbadala wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole,wakati akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya usajili kwa waganga wa tiba asili zaidi ya 37 wanaofanya kazi zao katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Dkt Mkasange alisema,lengo la Serikali ya Tanzania kuruhusu tiba asili na mbadala kufanyika bila kificho ni kutaka waganga hao waisaidie serikali yao katika kupambana na kutokomeza baadhi ya magonjwa ambayo yanahitaji tiba za asili kwa ajili ya kuokoa jamii ya Watanzania.
Dkt Mkasange alitahadharisha kuwa,udanganyifu unaofanywa na baadhi ya waganga kwa lengo la kujipatia fedha ni kosa kisheria ambapo amewataka kufanya kazi zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi yetu.
Aidha Dkt Kihongole,amewataka Waganga hao kufanya kazi kwa umoja na kushirikiana na Serikali yao katika mapambano dhidi ya adui maradhi katika jamii badala ya kujitenga.
“kuna tatizo la kuoneana wivu miongoni mwenu,mmejengeka na roho za husuda badala ya kushirikiana,pia kuna tatizo la kutoa siri za wagonjwa wenu,nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kuhusu tabia hiyo,nawaomba sana suala la kutunza siri za wateja wanaofika katika maeneo yenu ni jambo muhimu sana”alisema.
Pia,amewataka kufanya kazi kwa kujiamini na kuacha tabia ya woga au kufanya kazi kwa kujificha kwani inawanyima nafasi ya kufahamika na kuaminika na hata kuwatia hofu wateja wao.
Alisema,Serikali inatambua na kuthamini sana tiba asili baada ya kuona jamii kubwa ya Watanzania wanaamini tiba hizo katika kuponya magonjwa mbalimbali.
Dkt Mkasange,amewaonya kuepuka tabia ya kuwakumbatia wagonjwa kwani sio wote wanaofika katika vilinge vyao wanaweza kupona kwa tiba za asili bali wanahitaji tiba za Kisayansi zinazotolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za matibabu.
Kwa mujibu wa Dkt Mkasange, baadhi ya wagonjwa wanaokwenda kwa Waganga wa tiba asili wanakwenda kwa bahati mbaya na matatizo yao hayahusiani kabisa na tiba asili,bali wanalazimika kwenda huko kama sehemu ya kutafuta majawabu ya shida zinazowakabili.
Alisema, tabia ya kukumbatia wagonjwa ni hatari kwa kuwa baadhi yao wana magonjwa ya kuambukiza kama kifua kikuu, kwa hiyo ni vyema Waganga kuwa na tabia ya kutoa rufaa kwa wagonjwa wenye maradhi ambayo yameshindikana kupona kwa kutumia tiba za asili.
Baadhi ya Waganga wa tiba asili,wameishukuru serikali kupitia wizara ya afya kuwapatia vibali hivyo kwa kuwa vitawasaidia kufanya kazi zao bila kificho na kupata nafasi ya kwenda mikoa mbalimbali hapa nchini.
Dalia Omari,ameiomba Serikali kuwachukulia hatua waganga wanaofanya kazi zao kinyume cha sheria ikiwamo upigaji wa ramli chonganisha ambazo zinaleta mtafaruki katika jamii.
Mohamed Yasini(Tapata)anayefanya shughuli za tiba asili katika kijiji cha Mbesa amekiri kuwepo kwa vitendo vya utapeli na vitisho vinavyofanywa na wenzao na kuiomba serikali kutowafumbia macho watu hao kwani licha ya kwenda kinyume pia wanachafua taaluma na kazi ya tiba asili.