Mgeni Rasmi, kwenye Maadhimisho ya Juma la Elimu kitaifa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Sauda Mtondoo (kulia) aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, akiongozana na Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga (kushoto) walipokuwa wakitembelea mabanda kwenye hafla ya uzinduzi wa Jumala Elimu iliyofanyika Viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge wilayani Igunga.
UONGOZI wa Mkoa wa Tabora umeushukuru Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) pamoja na wanachama wake kwa kuchagua shughuli za Maadhimisho ya Juma la Elimu kitaifa kwa mwaka huu 2022 kufanyika wilayani Igunga, ikiwa ni kushirikiana na wanajamii kutatua changamoto zinazokabili sekta ya elimu wilayani humo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora kupitia, kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Sauda Mtondoo aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa kwenye hafla ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Juma la Elimu iliyofanyika Viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge wilayani Igunga.
Akizungumza katika hotuba ya uzinduzi alisema; Tunawashukuru Mtandao wa Elimu, TENMET kwa kuichagua Igunga kuwa sehemu ya kufanyia shughuli hizi za kielimu na ninawashukuru pia mimi binafsi kwa kunipa heshima ya kuwa pamoja nanyi katika kufungua mkutano huu muhimu wa maadhimisho ya Juma la Elimu..,”
Aliongeza kuwa shughuli za maadhimisho hayo yanatoa fursa muhimu ya kutafakari kwa pamoja jinsi ya kuendelea kuondoa vikwazo vya ujifunzaji na uimarishaji wa elimu kwa kiwango cha ujenzi wa umahiri/ujuzi wa utendaji.
Alisema kama Serikali itaendelea kushirikiana na TENMET katika safari ya kuboresha elimu hapa Tabora na Tanzania kwa ujumla.
Awali kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga akizungumzia shughuli za maadhimisho kwa mwaka huu, alisema wamedhamiria kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuchangia uboreshaji wa elimu nchini.
Pia kuhamasisha na kukumbusha jamii, serikali, mashirika yasiyoya kiserikali na wadau mbalimbali wa elimu kuhusu umuhimu wa uchangiaji wa elimu kwa kuzingatia kauli mbiu isemayo: Gharamia Elimu Bora Kuboresha Matokeo ya Ujifunzaji: Elimu Kwanza. Pamoja na hayo, ni kuhamasisha serikali kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na pia kuzingatia makundi yaliyokosa fursa kama watoto wenye ulemavu, watoto wakike na makundi mengine maalumu.
Hata hivyo, aliishukuru serikali kuu kupitia ofisi ya Raisi TAMISEMI na mkoa kwa kutoa kibali cha kufanyika kwa maadhimisho hayo ya Juma la Elimu kitaifa mkoani Tabora hasa katika wilaya ya Igunga.
“..Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kabisa kwa utayari wenu wa kutupokea tulipoleta ombi letu la kufanya maadhimisho haya hapa kwenu Tabora.
Kwa mwaka huu, zaidi ya mashrika yasiyo ya kiserikali 39 yenye wajumbe takribani 111 pamoja na Halmashauri yameshirikiana kuandaa maadhimisho hayo, huku wakilenga kutatua changamoto zinazokabili elimu Wilayani Igunga. Hii ni pamoja na kupanga mikakati endelevu ya kuondoa kabisa changamoto za uhaba wa madarasa, walimu, madawati, vyoo vya wanafunzi na walimu, pamoja na nyumba za walimu.
Baadhi ya Mashirika wanachama wa Mtandao wa Elimu Tanzania ni pamoja na Uwezo Tanzania, HakiElimu, Brac Maendeleo, REPSI, ADD International, ShuleDirect, Sense International, Malala Fund, WOWAP, Right to Play, CAMFED, WeWorld, Shule Bora, CASEE, AMUCTA, Pestalozzi Children’s Foundation, SAWO, CDO, Education Opportunity, Room to Read, Plan International, Lyra in Africa na Feed the children.
Wengine ni; KCBRP, CBIDO, KESUDE, KARUDECA, DRS, Beyond Giving, Mama Kevina Hope Children Centre, SALVE Regina, SMD, AWPD, Caritus Rulenge, Brothers of Charity, EOTAS, NELICO, MDREO, Sengerema CDH, Lake Victoria Disability Centre, St. Justin Center for Child with Disabilities, Children in Crossfire, Room to Read, AFRIWAG naTEN/MET Secretariat.