**********************
– Wamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan Na Serikali kuwajali Na kushirikishwa.
– Waomba Mkoa usimamie uanzishwaji Saccos ya Machinga Mkoa.
– Waahaidi kushirikiana Na TRA kudhibiti walipa kodi.
– RC Makalla awaahidi kuyafanyia kazi Mapendekezo yote ya SACCOS Na uboreshaji maeneo wanayofanyia biashara.
– RC Makalla athibitisha mapato yamepamda baada ya machinga kupangwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla leo April 28 amepokea Mpango kazi ulioandaliwa na Machinga wa Mkoa huo uliosheheni Maoni na mapendekezo ya kuwezesha ufanyaji Biashara kwa ufanisi mkubwa zaidi ili kuleta Matokeo chanya.
Miongoni mwa Mambo yaliyowasilishwa kwenye Mpango kazi huo ni pamoja na Udhibiti wa majanga ya Moto, Maboresho ya maeneo walipopelekwa Machinga, Kulindwa kwa maeneo waliyoondoka ili yasivamiwe upya, Udhibiti wa masoko yasiyo rasmi, Uanzishwaji wa SACCOS ya Machinga, Ushirikiano kwenye udhibiti wa upotevu wa mapato, Uanzishwaji wa Machinga marathon kwaajili ya kuchangia Damu na Uwepo wa takwimu kamili ya idadi ya Machinga na kupatikana kwa ofisi ya Machinga.
Akizungumza wakati wa kikao Cha pamoja na Viongozi wa Machinga kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, RC Makalla amepokea kwa mikono miwili ombi la Mkoa kusimamia Uanzishwaji wa SACCOS ya Machinga ambapo ameunda Kamati itakayojumuisha Wataalamu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya na Viongozi wa machinga.
Aidha RC Makalla amesema miongoni mwa kazi ya Kamati itakuwa ni kufanya mapitio ya katiba, kuainisha sifa za mwanachama ili kujirudhisha.
Hata hivyo RC Makalla amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira walipohamishiwa Wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kuanzisha route za Daladala kuchochea Biashara ambapo ameelekeza hata Fursa za mikopo zitolewe kwa waliopo kwenye maeneo waliyopangwa.
Pamoja na hayo RC Makalla amesema tangu zoezi la kuwapanga vizuri Wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara holela lifanikiwe Mapato yamepanda kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es salaam Namoto Yusuph amemshukuru RC Makalla kwa kutenga muda wa kuwasikiliza ambapo wameomba Serikali iweke Mkazo kwenye suala la kuzuia na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia udanganyifu unaofanywa na Wafanyabiashara kwenye mashine za EFD na risiti za kusindikiza mzigo ambapo risiti moja inaweza kutumika kwenye mizigo mingi zaidi.