Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi akiongea na waandishi wa habari juu ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu raia wa Ethiopia
Wahamiaji haramu wakiwa chini ya ulinzi mara baada ya kukamatwa
********************************
Na Fredy Mgunda,Iringa.
Jeshi la polisi mkoa wa Iringa linawashikiria jumla ya wahamiaji haramu 34 kutoka nchini Ethiopia wakisafirishwa kuelekea nchini Afrika ya Kusini baada ya kuwakamata katika eneo la Kitonga wilaya ya Kilolo.
Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi alisema kuwa wamefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu hao kwa ushirikiano na idara ya uhamiaji mkoa wa Iringa.
ACP Bukumbi Alisema kando ya kukamatwa Kwa raia hao wa kigeni Jeshi la polisi linamshikiria dereva wa Lori Maulid Chinunga miaka 37 mkazi wa Dar es salaam aliyehusika kuwasafirisha raia hao wakigeni kinyume Cha sheria.
Alisema kuwa tarehe 27/04/2022 majira ya Saa 10:00 jioni, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Iringa eneo la Comfort-Kitonga Kata na Tarafa ya Mahenge, Wilaya ya Kilolo Mkoa wa Iringa, tulifanikiwa kumkamata dereva MAULID CHINUNGA miaka 37, Muislam Mmakua na Mkazi wa Dar es salaam akiwa anasafirisha Raia wa kigeni wapatao 34 kutoka Nchini Ethiopia wakitokea Mkoani Pwani kuelekea Tunduma mkoani Mbeya kwenye gari aina ya FAW yenye namba za usajili T 529 DXF na tela T 826 DXP mali ya kampuni MIGHTY LOGISTICS LTD, watuhumiwa wote wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na watafikishwa Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Akitoa taarifa za matukio ya uhalifu mkoani Iringa Kamanda Bukumbi amelitaja pia tukio la kukatwa Mtu mmoja mkazi wa Kalenga Wilayani Iringa aliyekamatwa na meno ya tembo aliyoyaficha katika korongo.
Alisema kuwa Mnamo tarehe 16/04/2022 majira ya Saa 10:20 jioni maeneo ya Bumila Kata ya Nzihi Tarafa ya Kalenga Mkoa wa Iringa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kikosi dhidi ya ujangiri (KDU) tulifanikiwa kumkamata ROMANUS MUTUTURI miaka 45, mhehe na mkristo, akiwa na vipande 02 vya Meno ya Tembo yenye thamani ya Tsh 35,189,122/= aliyokuwa ameyaficha kwenye korongo baada ya kupokea taarifa fiche kutoka mwananchi zilizowezesha kukamatwa kwake.
“Mwisho nitoe rai kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kuwa na utii wa sheria katika kipindi hiki tunapoelekea Sikukuu ya EID EL-FITR, wasiache nyumba zao bila uangalizi muda wote, watumiaji wa vyombo vya moto (magari, bajaji na pikipiki) njia kuu na maeneo mengine wawe na utii, pia wananchi waache kujihusisha na vitendo vya uhalifuna badala yake washirikiane na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kwa wakati ili ziweze kushughulikiwa” alisema ACP Bukumbi.