NA GODFREY NNKO
WATANZANIA wametakiwa kuthamini, kuheshimu na kuunga mkono kitendo cha kizalendo kilichofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimwa Samia Suluhu Hassan cha kuandaa filamu maalumu ya Tanzania Royal Tour kwa ajili ya kutangaza utalii wa Tanzania Kimataifa.
Lengo likiwa ni kuwezesha Taifa kupata watalii wengi wa kigeni ambao watatoa mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kufungua fursa za ajira.
Filamu hiyo ya dakika 56 inaonesha vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania Bara kama vile Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengenti,na Tanzania visiwani inaonesha hoteli za kitalii ikiwemo iliyopo ndani ya bahari huko Pemba.
Aidha, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiye kiongozi wa kutoa maelezo kuhusu vivutio hivyo kwa Peter Grenberg, ambaye ni mwanahabari nguli na mtozi wa filamu kutoka kituo cha televisheni cha CNBC nchini Marekani.
Wito huo umetolewa na Bw.Ombeni Pallangyo ambaye ni Mkurugenzi wa The Ombeni Foundation, Ombeni Africa Safaris,Banana House Garden Grill Arusha,Tandoori House Kitchen Arusha na The Bougainvillea Iliboru Kisiwani wakati akielezea kuhusu Uzinduzi wa Filamu ya Tanzania Royal Tour ambao utafanyika jijini Arusha Aprili 28, 2022 na viongozi mbalimbali kutoka mataifa ya ndani na nje ya nchi wakitarajia kushiriki.
Bw.Ombeni ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani amesema kuwa,kitendo cha Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuamua yeye mwenyewe kuandaa filamu hiyo kwa kupita katika hifadhi za Tanzania ni uzalendo wa kipekee aliouonesha kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Utalii nchini inaleta mapinduzi thabiti ya kiuchumi kwa Watanzania.
Amesema, kwa sasa kila mmoja anashuhudia matokeo ya kazi hiyo nzuri aliyoifanya yaliyoanza kupatikana.
Ameongeza kuwa, ziara ya Rais Samia katika mataifa mbalimbali aliyofanya ikiwemo Marekani ambako pia Uzinduzi wa Filamu ya Tanzania Royal Tour ulifanyika umezidi kuleta tija na kila mmoja anashuhudia matokeo yake na mapokeo chanya ya filamu hiyo kimataifa, kitendo ambacho ni ujasiri na uthubutu mkubwa uliofanywa na Rais Samia kwa maslahi mapana ya nchi.
“Rais Samia ni hodari sana, nimpongeze kwa ujasiri wake mkubwa wa kupita mbugani akiandaa filamu hiyo, amefanya kazi ya mtu mwingine kwa upendo wake wa dhati.
“Wamepita Mawaziri wengi nyuma wa Utalii, lakini hawakufanikiwa kuleta mabadiliko kutokana na kutokuelewa, kuwajibika na ubishi. Jambo hili lingekuwa limefanyika huko nyuma, lakini ni uthubutu wa hali ya juu wa Rais Samia kuamua kufanya hivyo kwa manufaa ya nchi, lazima tumpongeze sana.
“Kitendo cha Mheshimiwa Rais kuacha ofisi na majukumu yake kufanya kazi ya mtu mwingine ili kuonesha mfano bora ni cha kupongezwa na kuungwa mkono. Lazima kuona utalii unakuwa endelevu na pia kuwa na watu ambao akili zao zimechambuka na pia wana connection na Sekta ya Utalii, lazima nguvu ipelekwe mataifa ya nje watu waliko na kuambatana na watu wanaojua tunakwenda wapi,”amesema Bw.Ombeni.
Amesisitiza kwamba ili kuzidi kufanikisha suala la kukuza utalii nchini, watu wanahitajika watakaozidi kujituma kwa moyo wa dhati wakitumia vyema maarifa yao, ubunifu, kujitambua, na ushupavu thabiti wa kutembea sambamba na Mheshimiwa Rais Samia katika kufanikisha kwa ufanisi ukuzaji wa Utalii.
Aidha Bw.Ombeni ameziomba Balozi za Tanzania katika mataifa mbalimbali, zimsaidie Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele kuitangaza Tanzania na fursa zake katika kufanikisha kuifanya Sekta ya Utalii nchini izidi kuinufaisha Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Wakati huo huo, Bw.Ombeni Pallangyo amewashauri baadhi ya watumishi wa umma ambao wana jukumu la kuunganisha na kuimarisha umoja miongoni mwa jamii kuendelea kuwajibika kwa uaminifu na uwazi ikiwemo kuacha kasumba ya kufanya kazi kwa mazoe na wakati mwingine kuyatazama maslahi yao.
Amesema, tabia za baadhi ya watu wakiwemo askari wa Jeshi la Polisi zimekuwa zikiwapa hofu wawekezaji jijini Arusha, kwani wamekuwa wakitumia nafasi zao kutengeneza namna ya kujipatia fedha isivyo halali kwa kuwatengenezea wengine kesi ambazo haziwahusu ili kupatiwa chochote.
“Hivyo, nichukue nafasi hii kuwashauri ndugu zangu, tushikiarne kwa kufanya kazi kama timu moja, ili kuhakikisha Taifa letu ambalo mama yetu Mheshimiwa Rais Samia ameonesha njia ya kuwaletea Watanzania maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo hii ya utalii inatimia,”amesema Bw.Ombeni.
Bw.Ombeni amesema ataendelea kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Samia za kutangaza vivutio vya utalii kila kona ya Dunia yakiwemo matamasha mbalimbali na vipindi vya runinga ambavyo huwa anavilipia mara kwa mara nchini Marekani.
“Dhamira yangu ni kuhakikisha, vivutio vya Tanzania vinazidi kuwa neema katika jamii na kupaisha pato la Taifa, hivyo licha ya kutumia gharama zangu mwenyewe kuvitangaza vivutio hivyo duniani, pia nitaendelea kuwa mstari wa mbele kushiriki hatua kwa hatua katika miradi ya maendeleo,”amesema Bw.Ombeni.
Aprili 18, 2022 filamu ya Royal Tour ilizinduliwa jijini New York na Aprili 21, 2022 huko Los Angeles nchini Marekani ambapo Aprili 28, 2022 uzinduzi utafanyika jijini Arusha.