**************************
Na Joseph Lyimo, Simanjiro
WATOTO 46,000 wa Wilaya ya Simanijiro Mkoani Manyara, walio chini wa umri wa miaka mitano wanatarajia kupatiwa chanjo ya matone ya polio kwenye kata 18 za wilaya hiyo.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Simanijiro, Dk Aristides Raphael akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo amesema wazazi na walezi wa watoto hao wanapaswa kuwapeleka katika vituo vilivyotengwa.
Dk Raphael amesema chanjo hiyo ya ugonjwa wa polio inatokana na mlipuko uliotokea Malawi Februari 17 mwaka huu baada ya mtoto mmoja wa jijini Lilongwe kudhibitika kufa kwa ugonjwa huo.
Amesema watoto hao wa Simanjiro watapatiwa awamu ya pili hadi ya nne ya chanjo hiyo itayohusisha mikoa yote ya Tanzania bara kuanzia Aprili 28 hadi Mei mosi, Juni hadi Julai mwaka huu.
“Awamu ya kwanza imefanyika Machi 21 hadi 24 mwaka huu ikihusisha mikoa ya jirani na Malawi ya Ruvuma, Mbeya, Songwe na Njombe,” amesema Dk Raphael.
Amesema kutokana na mwingiliano ulipo na nchi hiyo jirani na ugonjwa huo unavyoenea kwa haraka ofisi ya Rais-Tamisemi kwa kishirikina na Wizara ya Afya na shirika la Afya Duniani imepanga kufanya kampeni ya chanjo kwa awamu nne.
“Tunaomba mtusaidie kuhamasisha wananchi kujitokeza kuwapeleka watoto chini ya umri wa miaka mitano katika vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kupata chanjo ya matone ya polio,” amesema Dk Raphael.
Diwani wa kata ya Terrat Jackson Ole Materi amesema atashirikiana na wenyeviti wa vijiji kuhakikisha wananchi wenye watoto wanaostahili chanjo hiyo wanashiriki.
Diwani wa kata ya Ngorika, Albert Msole amesema chanjo hiyo itakuwa na manufaa kwa jamii hivyo watahakikisha wanawapa taarifa wahusika wote wakapate chanjo.
Diwani wa kata ya Msitu wa Tembo Kaleiya Mollel ameishukuru serikali kwa kuhakikisha wananchi wenye watoto wa umri wa chini ya miaka mitano wanapata huduma hiyo.