Mwananchi wa Kijiji cha Tawi Kata ya Mbwara Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, Habiba Said na Wastara Habibu wakiwa wamebeba kokote za ujenzi wa tenki la maji kijijini kwao.
Na Selemani Msuya, Rufiji
UAMUZI wa Wakala wa Majisafi na Usafi
wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kupeleka Mradi wa
Maji Kijiji cha Tawi Kata ya Mbwara umetajwa kuwa fursa ya kiuchumi, maendeleo
na jamii kwa wananchi wa kijiji hicho.
RUWASA wamepeleka maji kijiji cha
Tawi ikiwa ni kutimiza kauli mbiu yao ya Maji Bombani na kumtua ndoo mama
kichwani, ambayo ni kutekeleza Sera ya Maji inayotaka kila mwananchi achote
maji kwa umbali usiozidi mita 400.
Mradi huo umefikishwa kijiji cha
Tawi kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya
Uviko-19, kwa fedha za mkopo usio na riba wa Sh. trilioni 1.3 kutoka Shirika la
Fedha la Kimataifa (IMF).
Akizungumzia mradi huo Mwananchi
wa kijiji cha Tawi kata ya Mbwara wilayani Rufiji mkoani Pwani, Wastara Habibu
amesema kwa sasa ana uhakika wa kipato, hali ambayo inamsaidia kutekeleza
mipango yake ya kifamilia.
“Mradi huu kwangu ni fursa za
kiuchumi, kwani naweza kujipatia huduma za kijamii kama kununua sabuni, nguo,
chakula na mengine,” amesema.
Mwanamama huyo amesema wamekuwa
wakitumia muda mwingi kutafuta maji katika mabonde ambayo sio safi na salama,
hivyo ujio wa mradi huu utawaondolea adha hiyo.
Naye Habiba Said amesema ameamua kushirikia
kazi ya kutekeleza mradi huo kwa kuwa ameweza kujipatia kipato cha uhakika.
Said amesema kitendo cha
kupatikana kwa maji kijijini hapo shughuli nyingi za maendeleo zitatekelezwa
kwa ufanisi.
“Mimi nimeamua kushiriki mradi
huu kwa sababu, unanisaidia kupata fedha ambazo zinasaidia familia yangu. Ila
ninamuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hatutamuangusha,” amesema.
Kwa upande wake Ramadhan Salum
amesema mradi huo umewapunguzia baadhi ya changamoto za maisha ambazo walikuwa
wanapitia.
Salum amewataka vijana wanzake
kujitokeza kushiriki shughuli za maendeleo kwa faida ya kijiji na familia zao.
Naye Rajabu Salum alisema mradi
huo umewawezesha kuachana na kazi ya kukata mkaa ambayo ilikuwa inaharibu
mazingira.
“Miradi ya maji ilikuwa mijini,
ila sasa na sisi tumekumbukwa, tunaahidi kufanya kazi na kulinda mradi huu,”
amesema.
Mtendajii wa Kijiji cha Tawi,
Abdallah Kilimba amesema amefanya kazi kijijini hapo kwa miezi 10 ambapo
ameshuhudia wananchi wakiteseka kupata maji.
Kilimba amesema changamoto ya maji
kijiji cha Tawi kimesababisha wananchi wengi kuhama katika makazi yao ya asili
na kuhamia mabondeni.
“Tumejipanga vizuri kupitia
kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha mradi huu unalindwa ili uwe endelevu
kwa vizazi vijavyo. Hii kwetu ni neema ya kiuchumi, kijamii na maendeleo,”
amesema.
Meneja wa RUWASA, Wilaya ya
Rufiji, Mhandisi Tluway Ninga amesema wananchi wa Tawi wamekuwa wakiteseka
kutafuta maji safi na salama kwa takribani miaka 38 ila ni imani yao mwishoni
mwa mwezi Mei watakunywa maji safi na salama.
Mhandisi Ninga amesema Mradi wa
Maji Tawi ulisanifiwa mwaka 2020/2021 ambapo wamepokea Sh.milioni 562
kuutekeleza kwa muda wa miezi sita.
Amesema mradi huo unahusisha
ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 75,000, utasambazaji wa mabomba kilomita 11.52,
ujenzi wa ofisi ya kamati ya maji, nyumba ya kuweka pampu na vituo 13 vya
kuchotea maji ambapo hadi sasa wapo zaidi ya asilimia 40 ya utekelezaji.
“Sisi hapa mradi huu unaelekea
mwisho kwa sababu tumeshakamilisha kazi muhimu kama kusambaza bomba, ujenzi wa
vituo, nyumba ya pampu na kamati ya maji. Ujenzi wa tenki utakamilika ndani ya
wiki chache zijazo,” amesema.
Mhandisi huyo amesema mradi huo
ukikamilika utawezesha kijiji cha tawi kupata maji safi salama kwa asilimia 92,
ila kiwilaya watafikia asilimia 89 ikiwa ni sawa na kata 13, vijiji 34 kati 38
na vitongoji 56 kati 78.
Ninga amesema mradi huo
utanufaisha 1,270 katika, 1,385 wa vitongoji vyote vilivyopo kijiji cha Tawi.