SERIKALI imeombwa kutenga fedha za dharura kwa ajili ya kujenga angalau kilomita 70 kwa kiwango cha lami za barabara ya Mtara-Newala-Masasi hadi Songea kutokana na umuhimu wa barabara hiyo kiusalama.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni leo April 27,2022 jijini Dodoma Mbunge Nanyamba(CCM), Abdallah Chikota,amesema ni vyema serikali ikafanya jitihada za haraka za kuimarisha barabara hiyo ambayo ni muhimu katika suala zima la usalama.
Akijibu swali hilo,Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya, amesema barabara ya ulinzi ya kutoka Mtwara – Newala – Masasi hadi Songea yenye urefu wa kilometa 358, inaambaa na Mto Ruvuma.
‘Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa sasa inaendelea kuifungua barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe na ujenzi wa madaraja makubwa na madogo katika mito na mikondo ya maji inayokatisha barabara ipitike.”amesema Mhe.Kasekenya
Aidha ameeleza kuwa kilometa 208 zimefunguliwa na daraja kubwa la Mbangala (mita 120) mkataba wa ujenzi umesainiwa tarehe 11 Aprili, 2022 na baada ya kuifungua barabara yote Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.