WANANCHI wa Kijiji na Kata ya Shishani wilayani Magu,wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Salum Kalli, wameadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kujitolea kuchimba msingi wa jengo la Mama na Mtoto la kituo cha afya.
Pia wananchi hao wamempongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuwaletea fedha sh.milioni 250 za tozo ya miamala ya simu kutekeleza mradi huo utakaohudumia wagonjwa 33,822 kutoka wagonjwa 6,588 wa sasa.
Akizungumza jana kwa niaba ya wananchi hao,Diwani wa Kata ya Shishani (CCM) John Ngagaja,alisema wanamshukuru Rais Samia kutoa fedha kutekeleza mradi huo utakaoboresha huduma za afya ya mama na mtoto wakiwemo wananchi wa vijiji vya kata hiyo.
“Mkusanyiko wa wananchi walijitokeza kuchimba msingi wa mradi huu ni ishara ya kuupokea,kumshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuwaletea fedha na kuwasogezea huduma karibu, tutatibiwa hapa hapa sisi,wake na watoto wetu,”alisema.
Gangaja alisema awali serikali iliwaletea mamilioni ya fedha kutekeleza miradi wa afya ya mradi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD),upasuaji (Theatre)na kichomea taka na kuomba iwasaidie kuezeka maboma waliyoyajengwa kwa nguvu zao.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Shishani,Sara William pamoja na Musa Maganga(73) walisema mradi huo umewaondoa kwenye changamoto ya nauli na kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za mama na mtoto,utakapokamilika utakuwa mkombozi wao na utawawezesha kupata huduma karibu.
Kwa upande wake,Kalli alisema wananchi kuadhimisha miaka 58 ya muungano kwa kuchimba msingi wa mradi wa mama na mtoto na kuacha usingizi,wanaiunga mkono serikali ya awamu ya sita kwa vitendo kwa inayoyafanya kwa maendeleo yao.
“Niwashukuru kujitokeza kwenu kwa wingi kuja kushiriki mwanzoni mwa mradi huu,endeleeni na moyo huo, tushirikiane kwa uzalendo huo,umoja na utaifa wetu, CCM ilitupatia ilani kuhakikisha sekta ya afya inaboreshwa wananchi wanakuwa afya bora ndicho serikali kwa pamoja tunachokifanya hapa leo,”alisema mkuu huyo wa wilaya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Magu (DED),Federica Myovella alisema,serikali ilitoa sh.milioni 250 za ujenzi wa OPD, jengo la upasuaji na Insinlator, hivyo uhitaji wa wa majengo ya huduma za afya kwa wananchi wa Shishani awamu ya pili imeongeza sh.milioni 250 za kujenga jengo la mama na mtoto.