**************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Makamu Mwenyekiti wa Ccm Tanzania Bara ,Abdulrahman Kinana ameshauri vyombo vya serikali pamoja na viongozi kuwachukulia hatua wale wote waliotajwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma kwenye taarifa ya mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikalini (CAG).
Aidha amesema kuwa, endapo viongozi hao watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa haraka itasaidia Sana viongozi wengine kuchukua tahadhari na mambo hayo kutoendelea tena.
Ameyasema hayo hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza katika mkutano wake na viongozi pamoja na wanachama wa chama hicho uliofanyika mjini hapa.
Kinana amesema kuwa,wakati umefika wa serikali sasa kulifanyia kazi suala hilo ili kuziba mianya yote ya matumizi mabaya ya mali za umma ambazo zimekuwa zikitumika isivyo ,na kwa kufanya hivyo kunaweka nidhamu kubwa ya matumizi ya fedha za umma.
Aidha Kinana amewaonya wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho kuacha mara moja kugawa fedha kwa ajili ya kupata nafasi mbalimbali badala yake wafuate sheria na taratibu zilizopo.
Amewataka wagombea hao kufuata haki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani kama wamedhubutu kugombea ina maana wana uwezo mkubwa wa kuongoza .
“Naomba niwaambie wanachama kuwa mtu yoyote anayetafuta uongozi kwa fedha uongozi huo ni wake na sio wenu kwani ameununua kwa fedha hivyo inakuwa changamoto hata katika kuwatumikia wananchi “amesema Kinana.
Aidha amewataka wanachama hao wasipakane matope wakati wa uchaguzi kwani wakati huo ndio wagombea wengi huzushiwa jambo ambalo halipo kwa lengo la kuwakatisha tamaa ili wasigombee nafasi hizo,huku akiwataka kumpa kila mmoja haki yake na kuepuka uzushi.
Ameongeza kuwa, kuna viongozi wazuri sana ambao wana uwezo mkubwa wa kugombea na kuongoza ila wengi wao wanaogopa kutokana na kutokuwa na fedha ,hivyo kuwataka wanachama hao kutokubali kupokea fedha kwa ajili ya kuwachagua viongozi hao bali watende haki.
Naye Katibu Mkuu wa Ccm Taifa,Daniel Chongolo amesema kuwa , hivi sasa kuna ratiba ya uchaguzi katika mashina na matawi kwa jumuiya ambapo aliwataka wananchama mbalimbali kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwani hakuna mwenye haki ya kuchaguliwa zaidi ya mwingine.
Aidha amewataka wanachama hao kushikamana na kuwa kitu kimoja huku wakiacha majungu, fitina,uongo,na uzushi katika kipindi cha uchaguzi huku akiwataka kuacha kuchomekeana ili watu wote wapate haki zao za msingi.
“Moja ya changamoto kubwa katika kipindi hiki ni kuwepo kwa kiwanda cha kusema uzushi ,kutunga na kutengeneza watu ambao watawajali baadhi ya watu ,ambapo amewataka kuacha tabia hiyo badala yake waache watu wanaostahili wapewe uongozi badala ya kuweka watu wao katika nafasi hizo ili waweze kuwaendesha wao.”amesema Chongolo.
Mkuu wa mkoa wa Arusha ,John Mongela amesema kuwa,serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Hassan Suluhu wamefanya mambo makubwa ikiwemo sekta ya elimu ambapo shule 17 za sekondari zimejengwa kwa mkoa wa Arusha kitendo ambacho kimeongeza ufaulu kwa kiwango kikubwa .
Amesema kuwa,wameweza kujenga pia madarasa mbalimbali kupitia fedha za Uviko ambapo swala hilo limefanikiwa pia kujengwa kwa shule katika maeneo ya wafugaji na kuchochea swala Zima la elimu katika maeneo ya wafugaji.
Mongela amesema kuwa, kwa mkoa wa Arusha wameweza kupokea shs 4.7 bilioni katika maeneo mengi ikiwemo ujenzi za hospital , pamoja na ujenzi wa vituo 25 vya kutolea huduma za Afya zimaweza kujengwa katika awamu ya sita.
“Kati ya vijiji 390 vya mkoa wa Arusha tayari vijiji 304 Sasa vimefikiwa na mradi wa maji na hadi ifikapo 2025 vijiji vyote vitakuwa vimefikiwa na maji ,huku vijiji vingine vikifikiwa na umeme pamoja na kujengwa kwa barabara mbalimbali.
Naye Mbunge wa Arusha mjini,Mrisho Gambo amesema kuwa kwa kutambua mchango mkubwa unaofanywa na Rais Samia ameweza kukabithi bendera 1,500 kwa mabalozi wote wa matawi pamoja na kata zote pamoja na kukabithi Simu 25 kwa kata zote 25.
Aidha Mbunge huyo amekabithi pia spika 4 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za chama .
Amesema kuwa, pamoja na mafanikio mbalimbali bado kuna changamoto ya wamachinga kwani wengi wao hawana maeneo ya kufanyika shughuli zao hivyo kuomba kufanyika kwa tathmini kwa ajili ya wamachinga ili wote waweze kupata haki yao.
Hata hivyo aliomba kuruhusiwa kuuzwa kwa madini ya Tanzanite katika maeneo mengine ikiwemo mkoa wa Arusha badala ya biashara hiyo kufanyika katika eneo la Mererani pekee.