Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa hospitali ya CCBRT, Bi Brenda Msangi akizungumza katika mkutano na wanahabari juu ya tukio la kuchangisha fedha zitakazotumika kutoa huduma ya uzazi salama kwenye kitengo Chao kipya cha Afya ya Uzazi. Tukio hilo linatarajia kufanyia Mei 7, 2022 katika Hoteli ya Serana huku ikitarajiwa mgeni rasmi kuwa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete
Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa Serena hoteli, Bw. Seraphin Lusala ameipongeza CCBRT kwa kuendelea kutoa huduma bora zilizo na viwango, hivyo kwa kuwa Serena Hoteli ni mdau wa mkuu na wataendea kuwa bega kwa bega.
Mtaalam wa Mawasiliano wa Kampuni ya Coca Cola Kwanza Bw. Victor Byemelwa amesema kuwa kampuni yao inatambua umuhimu wa afya ya Baba, Mama na Mtoto hivyo inaendelea kuungana na CCBRT katika utoaji wa huduma bora.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi (Katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa Serena hoteli, Bw. Seraphin Lusala (Kushoto) na Mtaalam wa Mawasiliano wa Kampuni ya Coca Cola Kwanza Bw. Victor Byemelwa (Kulia) wakionyesha ishara ya mshikamano katika kuendeleza huduma ya afya mara baada ya kumaliza mkutano na wanahabari.
******************
Na Blasio Kachuchu – Dar es Salaam.
Katika kutatua changamoto zinazowakabili akina mama wajawazito walioko katika mazingira magumu na uzazi hatarishi, hospitali ya CCBRT kupitia kitengo chake kipya cha afya ya uzazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete wameandaa chakula cha usiku cha hisani kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazotumika kutoa huduma ya uzazi salama kwenye kitengo hicho.
Kitengo hicho chenye miundo mbinu maalum ya kuwahudumia wanawake wajawazito wenye ulemavu na wenye historia ya fistula au mabinti waliopata ujauzito wakiwa na umri mdogo ili kuhakikisha wanawake wote wanapata huduma ya uzazi salama.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi amesema kuwa CCBRT wana dhamira ya kuunga juhudi za Serikali za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi sambamba na kuzuia ulemavu.
“Ingawa kitengo hiki tunategemea kufunguliwa rasmi mwezi Juni, tumeanza kutoa huduma kwa awamu tokea mwezi Januari na kufikia sasa tumezalisha akina mama wajawazito wapatao 37. Kitengo hiki kitatumika kama hospitali ya rufaa ya kanda na tutakapoanza kutoa huduma kwa ukamilifu wake tutakuwa na uwezo wa kuwahudumia akina mama wenye ujauzito hatarishi wapatao 12,000 kwa mwaka”, amesema Brenda Msangi.
Bi. Brenda Msangi amewaomba wadau wote wa afya ya uzazi kuwaunga mkono ili kuwezesha mazingira ya uzazi yaliyo salama, yenye staha na ubora kwa mama zetu na kwamba ifike siku moja kila mwanamke aweze kutarajia ujauzito na kujifungua salama kwa furaha.
Katika hafla hiyo itakayofanyika jioni ya Mei 7, 2022 katika hoteli ya Serena Dar es Salaam mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu Mheshimiwa, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Kwa muda mrefu hospitali ya CCBRT kwa kushirikiana na serikali wamekuwa wakitoa huduma ya afya katika mifumo ya afya ya uzazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam, kujenga uwezo wa wataalamu wa afya walioko kwenye vitengo vya afya ya uzazi katika hospitali za umma za mkoa wa Dar es Salaam sambamba na ujenzi wa kitengo cha afya ya uzazi katika hospitali ya CCBRT.
Kwa upande wake wadau waliounga mkono hafla hiyo Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa Serena hoteli, Bw. Seraphin Lusala na Mtaalam wa Mawasiliano wa Kampuni ya Coca Cola Kwanza Bw. Victor Byemelwa wametoa ahadi kuendeea kuungana na CCBRT katika mapambano ya kuisaidia jamii katika suala la afya.