Mchezaji Bestina Kazinja (mwenye mpira) wa timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani akiumiliki mpira mbele ya Sharifa Mgoli wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Mambo ya Ndani wameshinda kwa magoli 86-12.Wachezaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) (kushoto) wakianguka katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake dhidi ya Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) katika michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. TPDC wameshinda kwa mivuto 2-0.
Mchezaji Hassan Mfuko (kulia) wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) akijaribu kuondoa hatari mbele Yusuph Hamad wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) katika mchezo wa soka wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. TRA wameibuka washindi kwa bao 1-0.
Niuka Charles (kulia) wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ametwaa ubingwa wa mchezo wa draft kwa wanawake kwa kumfunga Renalda Minde wa Wizara ya Afya katika michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
***********************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wamewavua ubingwa wa soka timu ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kwa kuwafunga bao 1-0 katika mchezo mkali na wa kusisimua wa michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa uliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Hatahivyo, bao pekee la TRA lilifungwa na Maxmilian Magwecho; ambapo timu hizo zilizokuwa zikishambuliana kwa zamu na kuonesha mchezo wa kiwango cha juu na kufurahisha mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo.
Katika mchezo mwingine timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii wamewafunga timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) kwa mabao 2-1 na kufanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali
Mabao yote mawili ya Maliasili yalifungwa na Newton Mlay na bao pekee la Uchukuzi lilifungwa na Stephano Meta aliyepata pasi safi toka kwa Idrisa Bahatisha.
Katika mchezo wa netiboli timu ya Uchukuzi SC wamewafunga Hospital ya Benjamin Mkapa kwa kuwafunga magoli 47-31.hadi mapumziko Uchukuzi waliongoza kwa magoli 27-16.
Nao timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani wamewapeleka puta timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kuwafunga magoli 86-12, washindi walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 18-4.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake timu za Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC), Idara ya Mahakama, Uchukuzi SC na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zimefuzu kwa hatua ya robo fainali itakayofanyika leo.
TPDC waliwaondosha Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa mivuto 2-0, nao Idara ya Mahakama waliwavuta Wizara ya Kilimo kwa 2-0; huku Uchukuzi SC waliwavuta Hazina kwa 2-0 na.TAMISEMI wakiwavuta Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa mivuto 2-0; nao kwa 2-0.
Kwa upande wa wanaume timu za Uchukuzi SC, Shirika la Maendeleo nchini (TPDC), Idara ya Mahakama na Wizara ya Mambo ya Ndani zimefuzu kwa hatua ya robo fainali baada ya kushinda mechi zao zote za hatua ya nane bora.
Timu ya Uchukuzi SC waliwavuta Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa 2-0; huku Idara ya Mahakama waliwaondosha Chuo cha Mipango na Maendeleo vijijini kwa mivuto 2-0; nao TPDC waliwavuta timu ya Wizara ya Kilimo kwa 2-0; na Wizara ya Mambo ya Ndani waliwavuta kwa kutoa jasho Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa mivuto 2-1, awali mchezo ulimalizika kwa sare ya 1-1 ndipo ukaongezwa mvuto mmoja na kupatikana mshindi.
Katika hatua nyingine, Salum Simba wa Kongwa DC na Niuka Chande wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wametwaa ubingwa wa mchedzo wa draft kwa wanaume na wanawake; nao Gervas Mashimaha wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mayasa Kambi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wamekuwa washindi wa pili; wakati Sophia Kambaya wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini na Samwel Mwakyoma wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) wameshika nafasi ya tatu
Michuano hiyo inaendelea leo kwa michezo ya bao kwa hatua ya robo fainali kwa michezo yakuvuta kamba, soka na netiboli, pamoja na mchezo wa bao.