Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WACHEZAJI wa timu za Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wametwaa ubingwa wa mchezo wa karata kwa wanaume na wanawake katika mashindano ya Kombe la Mei Mosi Taifa inayoendelea kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Mchezaji Jerald Ndamalahwa ameitwalia kombe TPDC baada ya kumshinda Enos Zilihona wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP); wakati Happiness Benedictor ambaye ni bingwa miaka miwili mfululizo ametwaa tena ubingwa huo kwa kumfunga Yusta Gerald wa Mzinga.
Ushindi wa tatu kwa wanaume umekwenda kwa Clement Makungu wa Wizara ya Madini baada ya kumfunga Salmon Kiyogele wa Taasisi ya Saratani Ocean Road; wakati kwa wanawake Ofarasia Muhoha wa Taasisi ya Saratani Ocean Road amekuwa wa tatu baada ya kumshinda Monica Cassian wa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Wakati huo huo; Timu machachari za Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Uchukuzi SC na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) zimefuvu hatua ya nane bora baada ya kuwafunga wapinzani wao katika mechi za jhatua ya 16 bora zilizofanytika kwenye viwanja vya Jamhuri pamoja na Shell Complex jijini hapa.
TANESCO ambao ni mabingwa watetezi wamewafunga Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa magoli 2-1 mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Shell Complex jijini hapa, ambapo magoli ya washindi yalifungwa na Ibrahim Saidi na Ndete Maketa, huku la TEMESA lilifungwa na Dalgobert Albano.
Nayo timu ya TRA wamewachapa Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) kwa bao 1-0; wakati timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Uchukuzi SC wamefuzu hatua ya nane bora baada ya kuwaliza ndugu zao wa damu Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa bao 1-0 lililofungwa na nahodha Lugano Mwasomola.
Timu nyingine iliyofuzu hatua hiyo ni Wizara ya Maliasili na Utalii waliowafunga Hazina kwa bao 1-0 lililofungwa na Albanus Kakuru;
Michuano hiyo inaendelea leo kwa hatua ya nane bora kwa mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake timu ya Mahakama watacheza na Wizara ya Kilimo; timu ya TAMISEMI watakutana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road; TPDC watakutana na NCAA na Uchukuzi wacheza na Hazina; wakati kwa wanaume timu ya Mahakama itavutana na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini; huku Uchukuzi watacheza na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC); nayo Wizara ya Kilimo watavutana na Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) watavutana na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Pia timu za netiboli zitacheza hatua ya nane bora ambapo Uchukuzi watakutana na Benjamin Mkapa Hospital; Mambo ya Ndani watakunana na NCAA; huku Ikulu watapepetana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM); nao na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) watakutana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA)