Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu,akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria duniani ambayo yameadhimishwa kitaifa leo April 25,2022 jijini Dodoma.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akimkabidhi mama mjamzito chandarua chenye dawa ikiwa ni njia mojawapo ya kumkinga na maambukizi ya ugonjwa wa Malaria katika siku ya malaria duniani iliyoadhimishwa kitaifa jijini Dodoma.
Waziri wa afya Ummy Mwalimu akiangalia dawa pamoja na vifaa vya kupulizia katika madimbwi na sehemu za mazalia ya mbu zilizopo katika mabanda ya maonesho kwenye maadhimisho ya siku ya malaria duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.
………………………………………………..
Na. WAF-DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imeweka mpango mkakati maalum wa miaka mitano kuanzia 2021-2025 unaolenga kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Malaria duniani ambayo yameadhimishwa kitaifa jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema mpango Mkakati huo unalenga kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria nchini kutoka wastani wa asilimia 7.5 ya mwaka 2017 hadi kufikia wastani wa chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025.
“Mpango huu una mikakati mikuu mitatu ambayo ni udhibiti wa mbu waenezao Malaria, uchunguzi, tiba na tibakinga ya Malaria kwa makundi maalum; na ufuatiliaji na tathmini ya mwenendo wa ugonjwa wa Malaria hapa nchini”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema katika kipindi cha mwaka 2021 jumla ya vyandarua milioni 7.5 vyenye dawa vimegawiwa kwa wananchi kupitia kliniki za wajawazito na watoto, shule za msingi za Umma na kupitia kampeni maalum ya usambazaji na ugawaji wa vyandarua katika kaya.
Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa zaidi ya nyumba 568,000 zimepuliziwa viuatilifu ukoko kwenye kuta ndani ya nyumba na hivyo kuwakinga zaidi ya watu milioni 2 dhidi ya maambukizi ya Malaria katika Halmashauri za Kakonko, Kasulu na Kibondo pamoja na Kambi za wakimbizi za Nduta, Mtendeli na Nyarugusu kwa Mkoa wa Kigoma; Halmashauri ya Biharamulo kwa Mkoa wa Kagera; Halmashauri ya Ukerewe kwa Mkoa wa Mwanza na Halmashauri ya Bukombe kwa Mkoa wa Geita.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Serikali imeendelea kununua na kusambaza vitendanishi na dawa za kutosha za kutibu Malaria katika vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo vipimo na matibabu ya Malaria yanatolewa kwa wananchi bila malipo na upatikanaji wake ni asilimia 98.
Kwa upande wa upatikanaji wa dawa, Waziri Ummy amesema Serikali imekua ikifuatilia ubora na usalama wa dawa za Malaria na kujiridhisha kuwa ni salama na zina uwezo wa kutibu kwa zaidi ya asilimia 96.
Waziri Ummy amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutekeleza afua mbalimbali za kutokomeza Malaria zimeweza kupunguza vifo kwa asilimia 71, kutoka vifo 6311 mwaka 2015 hadi vifo 1909 mwaka 2021. Kupungua kwa idadi ya wagonjwa waliothibitika kuwa na Malaria kwa asilimia 43 kutoka wagonjwa milioni 7.7 mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa milioni 4.4 mwaka 2021.
Mwisho Waziri Ummy amewataka wananchi kuendelea kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya Malaria kwani ugonjwa huu ni hatari kwa afya na maendeleo ya ustawi wa Taifa.