Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohammed Mussa (kulia) akiangalia Jiwe la Msingi la Jengo la Hanga la Ndege la Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST) baada ya Kufungu, Hafla iliyofanyika katika Taasisi hiyo Mbweni Mjini Zanzibar.
Mkuu wa Idara ya Uhandisi Mitambo na Magari kutoka Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), Ali Hamadi Mkali akielezea kuhusu Mashine ya Ndege inayotumika kwa Mafunzo ya Wanafunzi wa fani ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege, katika hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Hanga la Ndege , huko Mbweni Mjini Zanzibar.
Muonekano wa Jiwe la Msingi la Jengo la Hanga la Ndege la Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), lililofunguliwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohammed Mussa, huko Mbweni Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknoloji Zanzibar (KIST) Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi akizungumza katika hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Hanga la Ndege la Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), huko Mbweni Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bahati Geuzye akitoa salamu za Mamlaka hiyo, wakati akizungumza katika hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Hanga la Ndege la Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), huko Mbweni Mjini Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohammed Mussa akizungumza na Wafanyakazi pamoja na Wanafunzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), Baada ya Kufunguwa Jengo la Hanga la Ndege la Taasisi hiyo, huko Mbweni Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Wafanyakazi na Wanafunzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST), waliyohudhuria hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Hanga la Ndege la Taasisi hiyo, huko Mbweni Mjini Zanzibar.
PICHA NA MARYAM KIDIKO – KIST.
………………………………………….
Na Issa Mzee- KIST
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh Lela Mohammed Mussa, amesema Serekali inatambua mchango wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia(KIST), katika kuboresha maisha ya vijana na kulisaidia Taifa katika kuleta wataalamu wenye uwezo wa kutatua changamoto za kiufundi nchini.
Alisema Taasisi ya Karume inategemewa kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha malengo ya sera ya nchi hususan katika maendeleo ya viwanda,sera ya uchumi wa buluu pamoja na ukuaji wa teknolojia.
Alieleza hayo wakati wa ufunguzi wa Hanga la Matengenezo ya Ndege lililojengwa katika Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia(KIST), Mbweni Mjini Zanzibar, linalotarajiwa kutumiwa na wanafunzi wanaosoma fani ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege katika Taasisi hiyo.
Alieleza kuwa, hivi sasa Dunia inategemea Teknolojia katika harakati mbalimbali za maendeleo, hivyo Serekali inaendelea kuwakaribu na Taasisi ya Karume ili kuhakikisha Zanzibar inaenda sambamba na Dunia katika ukuaji wa teknolija kwa lengo la kuboresha maisha ya wananachi kwa vitendo.
Alisema Serikali ya awamu ya nane chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi inakusudia kuboresha maisha ya Wazanzibari wote kwa vitendo na hili linathibitishwa na sera zilizobora na zinazotekelezeka za serikali hii.
“Tunategemea kwa kiasi kikubwa wahitimu wote watakao maliza masomo yao katika Taasisi hii katika fani ya Uhandisi wa Matengenezo ya ndege wataisadia serikali, na watakuwa na uwezo wa kuajirika na mashirika mbalimbali nchini, na hata nje ya nchi”. Alisema Waziri.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaasa wanafunzi wanaotarajiwa kutumia hanga hilo kutunza vifaa vilivyomo, ili viweze kudumu kwa muda mrefu ili vizazi vijavyo viweze kunufaika.
Katika hatua nyengine Waziri Lela ameahidi kufanya jitihada za kina za kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali itakayopatikana inaelekezwa katika Taasisi za elimu ikiwemo Taasisi ya Karume.
Nae Mkuregenzi wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia(KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab alisema lengo la ujenzi wa hanga hilo ni kuwawezesha wanafunzi wanaosoma fani ya Uhandisi wa matengenezo ya ndege kujifunza kwa vitendo, kuhifadhi vifaa, pamoja na kutoa nafasi ya kutosha kwa ajili ya mafunzo ya wanafunzi hao.
Alieleza kuwa, uwepo wa hanaga hilo katika Taasisi ya Karume utawawezesha wanafunzi kujifunza katika mazingira halisi yanayofanana nayale ambayo watakumbana nayo katika ajira zao baada kuajiriwa kwani ujenzi huo umezingatia masharti na vigezo.
Alifafanua kuwa mradi huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 362143791, umefadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Kwa kushirikiana na Taasisi Ya Karume Sayansi na Teknolojia(KIST) ambayo ilitoa shilingi milioni 62143791.
Aidha alitumia fursa hiyo kuishukuru Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kuufandhili mradi huo licha ya kuwepo changamoto wakati wa ujenzi, ikiwemo uadimikaji wa malighafi za ujenzi ikiwemo nondo, pamoja kuengezeka kwa bei ya badhi ya malighafi mara kwa mara, jambo ambalo lilipelekea kuengezeka kwa gharama za ujenzi huo.
Vilevile Dk.Mamhoud alisema licha ya kuwepo kwa hanga la ndege katika Taasisi yake bado Tasisi yake inampango wa kujenga jengo la ghorofa moja ambalo linaambatana na eneo la hanga kwa ajili ya madarasa na ofisi, ambazo zitatumika kuendesha mafunzo zaidi yanayohusiana na masuala ya usafiri wa anga.
Akitoa salamu za Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bahati Geuziye, alisema lengo la kufadhili mradi wa ujenzi wa hanga la matengenezo ya ndege kwa ajili ya wanafunzi wa Taasisi ya Karume ni kuongeza jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia ili kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake nchini.
Alisema kuwa, ufadhili uliotolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa Taasisi ya Karume, utasaidia kwa kiasi kikubwa jitihada za kuimarisha masomo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege kwa wanafunzi wa Tanzania.
“Usafiri wa Anga ni muhimu katika kufanikisha jitihada za serikali za kupiga hatua zaidi kiuchumi kwasababu Tanzania kwa sasa inajielekeza kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati” alisema Mkurugenzi huyo.
Alifafanua kuwa, ili nchi iweze kupiga hatua kiuchumi ni lazima iwe na mfumo mzuri na uliobora wa usafirishaji ikiwemo usafiri wa anga.
Pia alisema kupitia ufadhili huo wa serikali vijana wengi wataweza kunufaika na kupata fursa ya masomo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege kwa gharama nafuu.
Aidha alisema Mamlaka ya Elimu Tanzania, inajivunia kuwa ni sehemu ya mafanikio hayo, na kuahidi kuendeleza ushirikiano na Taasisi za Elimu ikiwemo Taasisi ya Karume, katika uboreshaji wa mazingira yakujifunza na kufundishia ili kufanikisha lengo la serikali la kutoa elimu bora kwa wananchi wake.