Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire akisisitiza jambo kwenye khafla ya Iftah aliyowaandalia wachezaji wa klabu hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) jijini Dodoma. Klabu hiyo inashiriki michezo ya Mei Mosi inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali.
Mwenyekiti wa Klabu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Andrew Magombana akiwasilisha taarifa mbalimbali za klabu hiyo kwa Katibu Mkuu wa sekta hiyo, Gabriel Migire (hayupo pichani) wakati wa hafla ya Iftah aliyowaandalia wachezaji na viongozi wa klabu hiyo, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Wakala wa Majengo nchini (TBA), jijini Dodoma.
Baadhi ya Wachezaji wa Klabu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) wakimsikiliza Katibu Mkuu wa sekta hiyo, Gabriel Migire katika kikao kabla ya hafla ya Iftah aliyowaandalia kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) jijini Dodoma. Klabu hiyo ipo Dodoma ikishiriki mashindano ya Kombe la Mei Mosi Taifa.
Baadhi ya Wachezaji wa klabu ya Uchukuzi wakigaiwa chakula cha Iftah kilichoandaliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) jijini Dodoma. Timu hiyo inashiriki mashindano ya Kombe la Mei Mosi Taifa inayofanyika jijini hapa.
Mweka Hazina wa Klabu ya Uchukuzi, Benjamin Bikulamchi (wa kwanza kushoto) akifurahia mambo mbalimbalii yanayoelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire (hayupo pichani) wakati ya hafla ya Iftah aliyoiandaa na kufanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) jijini Dodoma. Timu hiyo ipo jijini ikishiriki michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa.
Mchezaji wa mchezo wa karata Stumai Mbago (kulia) akichukua chakula tayari kwa kufuturu katika iftah iliyoandaliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) jijini Dodoma. Uchukuzi wapo jijini hapa wakishiriki michezo ya Kombe la Mei Mosi Taifa.
………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Gabriel Migire ameipongeza timu yake ya Uchukuzi SC kwa ushindi walioupata kwenye michuano ya Kombe la Mei Mosi Taifa 2022 inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali jijini hapa.
Migire amesema hayo katika hafla ya Iftahi aliyowaandalia wachezaji na viongozi wa klabu hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo nchini (TBA), ambapo amesema anatarajia ushindi mnono zaidi kwa michezo mingine ambayo inaendelea.
“Nimepata taarifa tayari tumepata medali nyingi katika michezo iliyoisha ya riadha na kuendesha baiskeli, na pia nafarijika Zaidi kusikia pia timu zetu zote za michezo ya kuvuta kamba, netiboli na soka zimeuvu kwa hatua ya pili ya nane na 16 bora, nawaombea kwa Mungu muweze kutimiza lengo lililotuleta kwenye mashindano na tushinde kwa kishindo michezo yote na tutwae makombe mengi, mtakuwa mmenifariji sana nikiwa kama mlezi wenu,” amesema.
Hatahivyo, amewaagiza Wakuu wa taasisi zote zilizopo chini ya Sekta ya Uchukuzi kuithamini klabu hiyo na kuwa karibu nayo ili kuwatia moyo na ari ya ushindi kwa kuwa michezoinasababisha ufanisi mahala pa kazi kwani wafanyakazi watakuwa na afya bora na huondoa magonjwa nyemelezi.
“Nawaelekeza Wakuu wa Taasisi zote kuhakikisha wanatembelea kambi ya timu hii na kuzungumza nao ili kutoa hamasa ninaimani kwa kufanya hivyo watachagiza wimbi la ushindi na timu yetu itafanya vyema, pia wahakikishe wanatoa misaada inayohitajika ikiwemo ya ulipaji wa ada za mwaka kwa wakati na pia kuruhusu wafanyakazi wao mapema kipindi cha maandalizi ya michezo mbalimbali,” amesema Migire..
Halikadhalika amewahimiza Wakuu wa taasisi hizo kuhakikisha wanaendesha mabonanza yanayoratibiwa na wizara kila baada ya miezi minne, kwa kufanya mzunguko wa kila taasisi,
Kwa upande wa viongozi wa klabu hiyo amewaagiza kuhakikisha wachezaji wanaendelea na mazoezi ya mara kwa mara na sio kusubiri kipindi cha mashindano pekee, kwa kuwa itajenga timu bora yenye kuleta ushindani katika mashindano mbalimbali yakiwemo ya SHIMIWI, na pia itatimiza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan ya wafanyakazi wote wa Umma wafanye mazoezi kupitia mabonanza na kushiriki michezo, ili kuimarisha afya zao.
“NInawakumbusha kuwa kumalizika kwa mashindano haya ya Mei Mosi 2022 ndio mwanzo wa maandalizi ya michezo ya SHIMIWI 2022, hivyo niwatake muendelee na utaratibu wa kushiriki katika mazoezi binafsi mara kwa mara na msisubiri hadi pale uongozi unapotangaza msimu mpya wa maandalizi wa mashindano, kwa kuwa mwanamichezo bora hujiandaa wakati wote na sio kusubiri mazoezi ya zimamoto,” amesema Migire.
Amesema wizara yake ipo bega kwabega na timu hiyo na ameahidi itaendelea kununua vifaa mbalimbali zikiwemo jezi na baiskeli.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Andrew Magombana amesema klabu hiyo kwa sasa inaundwa na wafanyakazi 240 kutoka Wizarani pamoja na taasisi 13 zilizopo chini ya sekta ya Uchukuzi, na mpaka sasa mashindano yakiwa yanaendelea wamefanikiwa kupata ubingwa wa wanawake katika mchezo wa kuendesha baiskeli na wanaume wamekuwa watatu; huku katika mchezo wa riadha wamepata medali tatu za dhahabu, nne za Fedha nan ne za shaba.
Pia timu za soka imeingia hatua ya 16 bora baada ya kushinda mechi zake zote nne; pia netiboli imeshinda mechi zote tano na kuvuta kamba wanawake wameshinda mechi zote nne halikadhalika na wanaume wameshinda mechi zote.
“Tunakuhakikishia ushindi mkubwa Katibu Mkuu na hatutakuangusha tutatetea ubingwa wetu wa jumla tulioupata Mwanza mwaka 2021 kwa kuwa hadi sasa tunafanya vizuri katika mechi zaetu kwenye mashindano haya yanayoendelea na yatafikia tanati tarehe 29 April, 2022,” amesema Magombana.
MWISHO