**************************
Adeladius Makwega-DODOMA
Vijana wametakiwa kuwajibika na kutimiza majukumu yao kwa kanisa na taifa kwani kufanya hivyo ni kumtendea haki Kristo Mfufuka. Hayo yamesemwa na Padri Paul Mapalala Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Imakulata Chamwno Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma katika misa ya jumapili ya pili ya Pasaka iliyofanya kanisani hapo Aprili 24, 2022.
“Mara baada ya Yesu Kufufuka mitume walimuhubiri Kristo, wakati wao umekwisha, sasa ni wakati wetu, mimi na wewe. Wewe kama baba, wewe kama mama na wewe kama kijana unawajibika vipi kikanisa? Unawajibika vipi kumpeleka kristo katika mazingira tata na tatanishi? Hiyo ndiyo kazi ya wakati wetu wa sasa.” Alisisitiza Padri Mapalala.
Sasa ni wakati wa utandawazi, Je simu zinatumiwa vipi katika utandawazi huo? Simu yako unaitumiaje. Hapo kinachotazamwa ni uwajibikiaji wako, kama kijana, kama baba, kama mama, idadi kubwa ya Watanzania ni wazee? Au Vijana ? (Aliuliza), Ni vijana! (Alijibu).
“Kazi zingefanyika vizuri zaidi kwani vijana wana nguvu na wana akili timamu.” Alisema.
Kristo alifariki akiwa kijana, kutokuwajibika ukiwa mkristo kijana ni kumdhalilisha kristo, iwe katika mazingira yoyote yale, aliongezea padre huyo.
Misa hiyo ambayo ilikuwa ya kwanza inayoanza saa 12, 00 asubuhi ya kila jumapili, vijana walionekana kuwa watulivu mno huku wakimsiliza padri wao kwa umakini mkubwa na wakati wa kutoa sadaka kiongozI mmoja wa kanisa alisimama katika marufaa ya kanisa hilo huku akisisitiza yote aliyoyasema Padri Mapalala kwa vijana.
“Vijana tunapaswa kubadilika kabisa na ifahamike wazi sisi vijana ni umri kati ya miaka 18-45.” Alizungumza kiongozi huyo wa waamini parokiani hapo.
Wakati misa hiyo inaendelea kwaya ya vijana ilimba nyimbo zinazofahamika kwa waumini wote kwa uchangamfu mkubwa ambapo kwaya hiyo ilikuwa na wapiga kayamba wawili, mpiga kinanda mmoja, mwongozaji mmoja na wanakwaya 22.
Mwandishi wa ripoti alishuhudia vijana walipokuwa wakitoka kanisani baada ya misa hiyo wakisema bayana kuwa leo Baba Paroko amekuwa mkali sana.