Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Chamwino na Kongwa katika kikao cha dharura kutokana na mgogoro wa mipaka ya ardhi uliojitokeza baina ya pande hizo mbili.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remedius Emmanuel akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kongwa na Chamwino katika kikao cha dharura.
Kiongozi wa Wafugaji Wilaya ya Kongwa Moringe Parok akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka (hayupo pichani) kwenye kikao cha hadhara baina ya Wafugaji kutoka Wilaya ya Kongwa na Wakulima Wilaya ya Chamwino
Baadhi ya Wafugaji kutoka Wilaya ya Kongwa waliojitokeza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye kikao hicho ambao ni wakulima kutoka wilaya ya Chamwino, Mkoani Dodoma
………………………………
Na Bolgas Odilo, Dodoma.
WAFUGAJI Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma wametakiwa kupima maeneo yao wanayomiliki bila kuwa na hati miliki kutoka serikalini kufuata taratibu za kupata hati za umiliki wa maeneo yao na wayatumie kama sehemu ya malisho ili kuepuka migogoro.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka wakati akizungumza na wafugaji Wilaya ya Kongwa kufuatia mzozo wa ardhi uliojitokeza baina ya wafugaji kutoka wilayani humo na wakulima Wilaya ya Chamwino kijiji cha Wali.
“Kila mfugaji mwenye eneo lake ahakikishe anapima na kupata hati za kumiliki eneo hilo kutoka serikalini, bila kufanya hivyo hilo eneo linakuwa sio lako ni la serikali.
“Ukishapima eneo lako na ukapata hati unaweza kuchungia mifugo yako ndani ya eneo lako na unaweza ukaweka kisima na josho ili kuepuka hii migogoro isiyo na lazima na inaweza kuepukika.
“Acheni kuchungia mifugo yenu kwenye mashamba ya watu na kama mtaendelea kuchungia mifugo yenu kwenye mashamba ya watu mtaleta tena ugomvi mwingine,” alisema Mtaka.
Aidha Mtaka ameagiza wataalamu wa kupima mipaka waanze zoezi la kupima maeneo ya mpaka kati ya Wilaya ya Kongwa na Chamwino kuanzia Alhamisi wiki ijayo (28 April, 2022).
Kwa upande wao wananchi wa wilaya hizo mbili Chamwino na Kongwa wameridhishwa na maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka na kuwa tayari kwa utekelezaji.