MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amesema wakati Taifa linaenda kutimiza miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar April 26,2022, Chama Cha Mapinduzi (CCM),kimedhihirisha kuwa kina uwezo wa kutosha wa kuendesha nchi na kuwaletea wananchi maendeleo kupitia Sera na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Kutokana na hilo amevishauri vyama vya upinzani vijifunze kwa CCM ambao wameonyesha ukomavu wa kisiasa.
Akizungumza April 22,2022,na wanachama wa Shina namba 12 lililopo tawi la Ikungi A mara baada ya kupiga kura ya mwenyekiti na wajumbe wa shina hilo,Mtaturu amesema vyama hivyo vinapaswa kujifunza kwa chama kikongwe CCM.
“Hawa watoto bado wanatakiwa walelewe na mtoto ili umjue ana afya ni lazima aseme seme ,lakini suala la kuwapa madaraka bado sana,vyama hivi vijipange vianze kujifunza kwa CCM ambao ni baba lao na wanakaribia kutimiza miaka miaka 50,
“Leo tunawasikia mara wanaanzisha sijui CHADEMA Msingi sasa niwaambie kama unataka kujenga msingi imara ni lazima ujue namna unavyoujenga,na usipojenga msingi huo imara nyumba haiwezi kuwa nzuri hivyo wasiogope kujifunza kwa chama chenye uzoefu mkubwa,”amesema Mtaturu.
KAULI YA KUIBIWA KURA.
Akizungumzia hilo Mtaturu amesema CCM haiwezi kuiba kura kwa kuwa tayari ina mtaji wa wanachama wa kutosha kuanzia kwenye mashina hadi Taifa.
Ametolea mfano Wilaya ya Ikungi kuna mabalozi 2,000 na kila balozi ana wastani wa wanachama 30 kwa maana ana kura 60,000 za kuanzia.
“Ukichanganya viongozi wa matawi,kata na wilaya changanya na jumuiya za chama zote tatu unapata wapi ujasiri wa kusema umeibiwa kura kwa takwimu hizi,sasa unasema tumeibiwa kura unaibiwaje kura wakati huna,sisi tumewapa takwimu na wao watupe,mimi niwaombe tuendelee kuwaambia sisi tuna mtaji wa kutosha,naomba msisikilize maneno ya barabarani,hivi kweli unaweza kuogopa kinyago ulichochonga mwenyewe,tulikubali wenyewe mfumo wa vyama vingi,hatuwezi kuogopa chama tulichokubali kianzishwe,
“Leo tunachagua viongozi wa mashina,lakini wenzetu wao hawaelewi hata mfumo huu jinsi ulivyo,sasa hizo kura wanazodai kuibiwa wanazitoa wapi,?amehoji.
MAFUNZO MASHINANI.
Mtaturu ameahidi kuhakikisha wanawajengea uelewa viongozi wa mashina waliochaguliwa katika jimbo la Singida Mashariki ili wajue wajibu na majukumu yao katika kukijenga chama ikiwemo kuwaunganisha wanachama.
“Katibu nikuombe sana tukimaliza uchaguzi tushirikiane tuandae mafunzo maalum kwa viongozi wetu,tuwajengee uwezo wajue wanaenda kufanya nini katika mashina yao,uhai wa chama unaanzia kwenye shina lako,je wanachama ulionao wapo hai,kwa maana wanalipa ada,
“La pili la kuzingatia je wanatimiza wajibu wao wa kikanuni wa kukisemea chama,wanafanya wajibu wao kuisimamia ilani ya uchaguzi kuona iliyotekelezwa,haya ndio maswali yanayopaswa kujibiwa kupitia mafunzo hayo maalum,”amesema.
ANUANI ZA MAKAZI NA SENSA YA WATU NA MAKAZI.
Ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wote kuendelea kushiriki zoezi la Anuani za makazi ikiwa ni maandalizi ya Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 2022,
“Zoezi hili ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu,niwaombe tuhimizane na tusikubali kuwa kikwazo Cha kukwamisha ufanisi wa zoezi hili maana faida zake tunazifahamu,zoezi hili litatambua pia maeneo yetu ya biashara na hivyo kuturahisishia katika upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha,tushiriki wananchi wenzangu,” amesisitiza.
KUHUSU UJENZI WA CHUO CHA VETA.
Mtaturu amesema akiwa Mkuu wa Wilaya aliwahi kufanya utafiti na kugundua kuwa kati ya watoto wanaomaliza masomo yao ni asilimia 20 pekee ndio wanaendelea na masomo ya juu na asilimia 80 iliyobaki wanabaki nyumbani.
“Hili ndugu zangu niliona ni bomu,kama kiongozi wa serikali nikasema hatuwezi kubaki kulalamika,na tunajua baba mzuri ndani ya nyumbe ni yule anayeondoa matatizo,nikaandika barua ya kuomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha Veta na nashukuru Rais wa awamu ya tano hayati Dkt John Magufuli aliridhia na kutoa Sh Bilioni 2 na ujenzi ukaanza,
Amesema tangu serikali ya awamu ya sita iingie madarakani wamepelekewa fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo ikiwemo Elimu, Afya,Umeme na Miundombinu ya barabara.
“Baada ya kuanza ujenzi kukatokea shida kidogo ya kimifumo lakini baada ya kurekebishwa ujenzi ukaendelea na hivi ninavyoongea unaenda kwa kasi na tumekubaliana mwezi Julai mwaka huu uwe umekamilika na vijana waende wakajifunze,tunamshukuru sana Rais Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifungua nchi na kuleta maendeleo nchini,”amesema.
Amesema dhamira yao ni kuona vijana wanaomaliza masomo yao na kushindwa kuendelea wapate ujuzi ili waweze kujiajiri na mikopo inayotolewa na Halmashauri isaidie kuwapa vifaa badala ya fedha.