NA FRED ALFRED,DODOMA
MAHAKAMA ya Tanzania imesema katika mpango mkakati wa awamu ya pili wa maboresho ya Mahakama nchini ambao ulianza 2020 hadi 2025 inatarajia kujenga Mahakama 10 za mwanzo za mfano katika maeneo ambayo ilikuwa ni vigumu wananchi kufikia haki.
Imesema kati ya Mahamaka hizo mbili zitajengwa Dodoma katika Kijiji Cha Kinusi wilaya ya Mpwapwa na Haubi Wilaya ya Kondoa.
Hayo yalibainishwa jana jijini hapa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel alipotembelea Kijiji cha Haubi Wilaya ya Kondoa.
Alisema Mahakama inaendelea na maboresho ambapo kwa mujibu wa mpango mkakati ulioanza tangu mwaka 2015 hadi 2020 ambapo mambo makubwa yamefanyika.
“Sasa tupo katika mpango mkakati wa awamu ya pili ambao umeanza 2020 hadi 2025, katika mpango mkakati huu kutakuwa na maboresho kwani hadi sasa Tanzania kuna Mahakama za mwanzo 960 huku mahitaji yakiwa ni 3900 hivyo bado kuna upungufu,”alisema.
Aliongeza kuwa:”Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Hamisi Juma katika vikao vyetu alielekeza kuwa ni vyema kuangalia namna ya kujenga mahakama za mwanzo kwa kuzingatia maeneo yasiyo pungua 10 ambayo ni vigumu wananchi kufikia haki na lengo la maboresho hayo ni kuhakikisha haki inapatikana kwa urahisi,”.
Profesa Gabriel alisema serikali itajenga jengo jipya la Mahakama ya mwanzo na Nyumba mbili za Watumishi.
Alisema katika kutekeleza hilo wanahitaji ardhi isiyopingua ekari mbili, uhamasishaji wa wananchi ili kuthamini kile kitakachojengwa, na kujitolea kwa wananchi kushiriki shughuli za ujenzi.
“Kitu ambacho ningetamani kusikia kutoka kwenu ni upatikanaji wa ardhi ambayo itamilikishwa kwa mahakama na mtuambie utayari wa wananchi kupokea jambao hili na kushiriki,”alieleza.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Haubi Paul Irovya, alisema ni kweli mahakama iliyopo ni ilijengwa muda mrefu kabla ya Uhuru na majengo yake yamechakaa yanahitaji matengenezo au ujenzi rasmi.
Alisema ujenzi wa Mahakama yenye hadhi itakuwa ni jambo jema kwasababu itawapinguzia wananchi mzigo wa kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta haki.
“Tunaishiuru serikali kwa maono yake na kuamua kujenga mahakama hapa haubi, tunaamini itakuwa na tija kwa wananchi wetu kwasababu itawarahishia na kuwapunguzia mzigo mkubwa waliokuwa wamebeba wa kusafiri umbali mrefu kwaajili ya kutafuta haki.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Haubi Anasi Lubuva alisema licha ya kuwepo kwa mahakama hiyo iliyochakaa lakini bado kunachangamoto ya kukosa Hakimu kwani aliyepo anahudumia Mahakama zaidi ya mbili.
Alitaja changamoto nyingine iliyopo katika kijiji hicho kuwa ni Mabalaza ya Kata yalipo hayana ujuzi namna ya kuenesha kesi, wakati mwingine wanaendesha kwa uzoefu sio kwa kufuata sheria hivyo ni vyema wakaandaliwa semina maalumu kwaajili ya kufundishwa namna ya kuendesha kesi.
“Tunachangamoto ya kukosa Hakimu na aliyepo anahudumia Mahakama zaidi ya mbili hivyo kunawakati wananchi wanakuwa wanamuhitaji lakini kutokana na majukumu anashindwa kufika, pia tunaomba semina itolewe kwa Mabalaza ya Kata ili waweze kutoa uamuzi kisheria zaidi,”alisema