Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Jumla ya watoto 200,967 waliochini ya miaka mitano mkoani Pwani wanatarajia kupata chanjo ya matone (POLIO) ili kuwajengea kinga na kuzuia kuenea kwa virusi hivyo .
Watoto hao wanatarajia kupatiwa chanjo hiyo kufuatia february17 mwaka huu nchi ya Malawi kutoa tamko la kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo , baada ya mtoto mmoja kutoka Mji Mkuu wa Lilongwe kuthibitika kuwa na ugonjwa huo.
Hayo yalisemwa na Mratibu wa chanjo Mkoa wa Pwani Abbas Hincha wakati wa kikao cha kamati ya afya ya msingi ya mkoa ,juu ya kampeni ya chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka mitano ,kilichofanyika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkoa.
Pia alieleza ,kampeni hiyo Ni ya nyumba kwa nyumba ,inachangiwa na nchi kuhofia kuwa kwenye hatari ya ugonjwa huo kuingia mara baada ya February 17 mwaka huu nchi ya Malawi kutoa tamko la kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo .
“Nchi ya Malawi na Tanzania kuna mwingiliano mkubwa wa kibiashara na huduma nyingine za kijamii hivyo hatari ipo na chanjo ni muhimu itasaidia kuzuia ugonjwa huo usienee ;”
Nae mganga mkuu Mkoani Pwani ,Dkt.Gunini Kamba alieleza , kwa mara ya mwisho Tanzania ilipata mgonjwa wa Polio Julai 1996 hivyo kampeni hii inatarajiwa kufanyika katika nchi zinazopakana na Malawi ikiwemo Zambia,Msumbuji, na Zimbabwe .
Alifafanua ,kampeni hiyo itaanza April 28 hadi Mei 1 mwaka huu watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano watachanja bila kujali chanjo alizopata siku za nyuma .
Kamba aliitaka ,jamii itambue usalama wa chanjo hiyo na wasiingie katika upotoshaji wowote kwani Ni Kama chanjo nyingine.
Vilevile alisema kuwa ugonjwa huo hauna tiba ila hukingwa na chanjo ya Polio ambayo ipo katika mfumo wa matone .
Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, mkuu wa wilaya ya Mafia , Martin Ntemo aliitaka jamii kuipokea kampeni hii na kutokuwa na hofu .
Ntemo alisema ,chanjo ni ileile inayotumika miaka yote lengo ni kuongeza kinga , kuzuia mlipuko na kudhibiti watoto wasipatwe na virusi vya ugonjwa huo.
Ugonjwa wa polio unasababishwa na kirusi cha polio ambacho huambukizwa kutoka kwa mtu alieathirika kwenda kwa mwingine kwa kunywa au kula chakula ama kinywaji kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea vya ugonjwa wa polio.
Virusi vya polio huzaliana katika utumbo na huweza kuathiri mfumo wa fahamu ikiwa ni pamoja na kupooza kwa ghafla kwa viungo ndani ya masaa machache hata kupelekea kifo .