Dk, Elizabeth Makamba akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
Dakitari wa magonjwa ya macho kutoka katika hospital ya rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sokouture Dk, Elizabeth Makamba akiendelea kutoa huduma ya upimaji wa macho
************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Imeelezwa kuwa wanawake wenye tabia ya kubandika kope kwenye macho wako kwenye hatari kubwa ya kupoteza uwezo wa kuona.
Hayo yamebainishwa na Dakitali wa magonjwa ya macho kutoka katika hospital ya rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sokouture Dk, Elizabeth Makamba wakati akizungumza na Fullshangwe ofisini kwake juu ya tabia ya baadhi ya wanawake kupenda kubandika kope.
Amesema kuwa kope asili ni sehemu moja wapo ya macho ambayo inapatikana kwenye kifuniko cha macho na kazi yake kubwa ni kulinda jicho, kurekebisha mwanga unaoingia kwenye macho.
Amesema kuwa macho ni kiungo laini sana ambacho hakiitaji kuchezewa ovyo ovyo hivyo kuweka kitu chochote kwenye jicho ambacho siyo kisafi kinaweza kusababisha kupata madhara makubwa ikiwemo kupoteza uwezo wa kuona.
Makamba amesema gundi zinazotumika kubandika hizo kope zinaweza kuleta aleji kwa mtumiaji kwa kupata muwasho,jicho kuvimba na hatiame kufanya macho yasione.
“Tabia ya ubandikaji wa kope bandia inaweza kuharibu mfumo mzima wa utengenezaji wa kope asili hali itakayopelekea uzalishaji wa kope kuwa mdogo na mwisho kujikuta hana kope kabisa”,amesema Makamba.
Kutokana na madhara hayo ambayo wanaweza kuyapata kwa kubandika kope Dk Makamba amewaasa watanzania kuyapenda macho yao ili waweze kuyatunza.
“Pindi inapotokea umepata ugonjwa wa macho msipende kutumia dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya ya macho,pia jengeni tabia ya kupima macho kila mwaka ili utakapogundulika na ugonjwa iwe rahisi kuanza tiba”,amesema Makamba.
Kwa upande wake Prisca Pius ambae ni mfanyakazi wa saluni ya Paint Me iliyoko Jijini Mwanza amesema kuwa kuna aina mbili za ubandika wa kope machoni ambazo ni Kope ya mkanda na kope ya moja moja.
Akifafanua aina hizo amesema kope ya mkanda haina madhara makubwa kutokana na aina ya kope hiyo kubandikwa bila gundi, lakini kope ya moja moja inamadhara kwasababu inatumia gundi ambapo wakati wa kubandua inaweza kutoka na kope za asili.
Pius amesema kuwa katika kipindi cha miaka tisa alichofanya kazi amekuwa na utatatibu wa kuwashauri wateja wake faida na hasara za uwekaji wa kope ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.