Na Selemani Msuya, Newala
BAADA ya miaka 60 ya wananchi wa kijiji cha Mandara wilayani Newala mkoani Mtwara kufuata maji umbali wa kilomita tatu, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA), wameondoa adha hiyo kwa kuwafikishia maji safi na salama bombani.
Aidha, wananchi hao wametoa shukurani kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kuonesha anawajali wananchi hasa wa vijiji kwa kuwapatia miradi ya maendeleo.
Wananchi hao wameelezea furaha hiyo kwa waandishi ambao wametembelea miradi inayotekelezwa RUWASA, kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, kwa fedha za mkopo usio na riba wa Sh.trilioni 1.3 za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Bishea Mohamed wa kijiji cha Mandara amesema wanashukuru RUWASA kuwapatia maji kupitia fedha za ustawi, hali ambayo itawahakikishi kunywa maji safi na salama na kuachana na maisha ya kuata maji kilomita tatu.
Mwanamama huyo amesema awali walikuwa wanafuata maji umbali wa kilomita mbili hadi tatu, hivyo ni wazi ujio wa mradi huo utawawezesha kujikita na shughuli za uzalishaji kama kilimo, biashara na nyingine.
“Maji ndio uhai wetu na sisi wanawake ndio kabisa, kwani tunatumia kupika, kufua, kuoga, kuosha vyombo na mambo mengine, kwa hiyo tunashukuru kwa kweli, tunachoomba haya maji yawepo kila siku kama ambavyo RUWASA wametuahidi,” amesema.
Amesema kutokana na kufuata maji mbali amekuwa akiumwa mara kwa mara. “Tulikuwa tunaenda mabondeni kufuata maji yaani tena kama mimi ambaye ninasumbuliwa na kifua, nilikuwa nikibeba ndoo moja tu kifua kinauma, ila mradi huu umeleta nafuu kwangu na wenzangu,” ameongeza.
“Ujumbe wangu kwa Rais Samia namwambia ahsante kwa kutuletea maji na tunakuahidi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 tutamchagua kwa kura nyingi ili aendelee kutuletea maendeleo Mandara,”amesema.
Naye Fatma Nawanji ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mandara amesema anaishukuru Serikali na RUWASA kwa kupeleka maji kwenye kijiji chao, hali ambayo itamuwezesha awahi shuleni.
“Naishukuru RUWASA kutuletea maji karibu na nyumbani, naamini sasa nitawahi shuleni, nikiwa msafi na hata uwezo wangu darasani utaongezeka,” amesema Fatma.
Kwa upande wake Shamira Mwaya amesema mradi huo wa maji umewaondolea mateso ya muda mrefu kutokana na kufuata maji mbali.
“Haikuwa kazi rahisi ndugu mwandishi kufuata maji Mitema, tulikuwa tunaumia maana unakuwa na mtoto mgongoni na maji kichwani, ila sasa na sisi tupo kama watu wa mjini,” amesema.
Abdallah Mohamed amesema kilichofanywa na RUWASA kijijini kwao ni cha kupongezwa na kuendelezwa jambo ambalo yeye na wenzake watashirikiana kulinda mradi huo.
Amesema walikuwa wanafuata maji na baiskeli kwa zaidi ya saa tatu, hali ambayo ilikuwa inakwamisha shughuli nyingine za maendeleo.
“Tumepata shida kwa miaka mingi, hakika leo tunashukuru Rais Samia na Serikali kutuletea maji kijijini kwetu, ikimpendeza tunaomba aje mwenyewe tumpe shukrani yetu,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mandara Ismail Lukanda amesema wanashukuru kupelekewa mradi wa maji kijijini kwao, kwani kipindi cha nyuma walikuwa wanapata shida.
“Tulikuwa tunaenda maili nyingi kufuata maji kwenye milima na mabonde, lakini sasa wananchi wangu watakuwa wanachota maji nyumbani. Tunampongeza Rais Samia na RUWASA ambao tumeshirikiana kwa pamoja hadi mradi huu umekamilika na sasa maji yanatoka,” amesema.
Lukanda amesema watautunza na kulinda miundombinu ya mradi huo kwa nguvu zote, ili uweze kudumu kwa muda mrefu.
Akizungumzia mradi huo Meneja wa RUWASA Wilaya ya Newala Mhandisi Nsajingwa Paul amesema miradi ya ustawi katika majimbo mawili Newala Mjini na Vijiji imepatiwa Sh.milioni 777.8 ambayo inatekelezwa na Kampuni ya Ukandarasi ya UR Investment.
Amesema miradi hiyo itaweza kuhudumia watu 10,021, ambapo kazi zinazofanywa ni kutandaza mabomba kilomita 44.2 na hadi sasa bomba zimesambazwa kilomita zaidi 25.
“Vituo vya kuchotea maji ni 24 na 13 vimeshajengwa, ujenzi wa tenki umefikia asilimia 50, pampu imeshafungwa. Miradi hii ikikamilika maji Newala yatapatikana kwa asilimia 63 kutoka asilimia 58 ya sasa,” amesema.
Meneja huyo ametaja vijiji vinavyonufaika na mradi huo ni Mandara, Kupete, Mnali, Chiunjila, Mkwedu na Mpipili.
Aidha, Mhandisi Paul ametaja miradi mingine wanayotekeleza ni Mradi wa Miyuyu Mlima unaogharimu Sh.bilioni 5.6 utakaonufaisha watu 22,990 na kuondoa kumaliza kero ya maji Newala Kaskazini.
Naye Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mtwara, Primy Damas amesema mkoa huo unatekeleza miradi ya ustawi katika majimbo tisa ambapo hadi sasa wamefikia asimilia 50 ya utekelezaji.
“Mkoa huu una wilaya tano ambapo miradi ya ustawi inatekelezwa majimbo mawili ya Wilaya ya Mtwara ambayo ni Nanyamba na Mtwara DC, Newala mawili, Masasi matatu, Nyanyumbu na Tandahimba kuna majimbo mawili.
Miradi hii tisa inagharimu Sh.bilioni 5.37 na ikikamilika itaweza kuhudumia watu 65,000 na kuongeza asilimia sita ya upatikaji maji, hivyo tutatoka asilimia 62 ya sasa hadi asilimia 68,” amesema.
Meneja huyo alisema pia kupitia mipango mbalimbali ya mkoa na wizara wanatarajia kupitia mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2025 lengo la maji vijijini asilimia 85 litafikiwa.
Mhandisi huyo ametoa wito kwa wananchi ambao miradi inatekelezwa katika vijiji vyao kutunza miundombinu hiyo ili iwe endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.