**************************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alhaji Abubakar Kunenge ameuagiza uongozi wa Chama kikuu Cha Ushirika Mkoani Pwani CORECU kuwachukulia hatua Kali za kisheria wale watakaobainika kuhujumu Chama hicho.
Sambamba na Hilo, ameupongeza uongozi wa mpito wa Chama hicho Kwa kusimamia zao la korosho ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 7 mwaka 2019/20 Hadi kufikia Tani 15 msimu wa mwaka 2021/22 na Daraja la kwanza la korosho kufikia Tani 72 ya Korosho zote.
Aliyaelekeza hayo, katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama hicho uliofanyika mjini Kibaha April 21,2022 katika ukumbi wa Shirika la Elimu Kibaha.
Kunenge alikitaka Chama hicho kiwe na utaratibu wa kuwajibishana endapo kiongozi ama Mwanachama anaenda kinyume na taratibu za Chama hicho.
Pia amewataka wakuu wa Wilaya kuwachukulia hatua ,wanaoenda kinyume bila kujali itikadi za Chama.
Katika hatua nyingine RC Kunenge Amesema mkoa na Wilaya umedhamiria kuleta mapinduzi katika Zao la Korosho.
“Tumedhamiria kuleta Mabadiliko katika Zao hilo la korosho ila peke yetu hatuwezi ni lazima tushirikiane katika hili.”alifafanua.
Vilevile aliwataka Wanachama wa CORECU wasifanye makosa katika kuchagua viongozi wapya baada ya uongozi wa mpito kumaliza muda wake.
Alisema endapo Chama hicho kikipata viongozi waadillifu ,wasimamizi Wazuri na watakaotosha Basi kitafanya vizuri katika majukumu yake.