Mchezaji Abubakar Ally wa timu ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) akijaribu kumpita Ramadhani Kalolo wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) wakati wa mechi ya soka ya michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Kilimani Park jijini Dodoma, ambapo TARURA walishinda kwa magoli 6-0.
Nahodha wa timu ya Uchukuzi SC, Lugano Mwasomola (kulia) akipiga mpira wa kichwa langoni mwa timu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika mchezo wa michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Kilimani Park jijini Dodoma. Uchukuzi ilishinda bao 1-0.
Mchezaji Nyamboge Mwita (WA) wa timu ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) akiwahi mpira huku Zitha Mndeme (WD) wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) naye akiuwania pia katika mchezo wa netiboli wa michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Kilimani Park jijini Dodoma. TRA ilishinda kwa magoli 36-12.
Kiungo hatari Aziza Mussa ( C) wa Wizara ya Maji akidaka mpira mbele ya Salome Mika wa timu ya Ofisi ya Rais Ikulu katika mchezo wa netiboli wa michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Kilimani Park jijini Dodoma. Ikulu walishinda kwa magoli 27-12
Wachezaji wa timu ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) (kushoto) wakiwavuta Tume ya Utumishi wa Walimu kwa mvuto 1-0 katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume wa kombe la Mei Mosi Taifa uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
…………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU za Wizara ya Mambo ya Ndani na Ofisi ya Rais Ikulu zimeendelea kugawa dozi kwa wapinzani wao katika michuano ya kombe la Mei Mosi kwa upande wa mchezo wa netiboli iliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Ikulu ambao ndio mabingwa watetezi waliwafunga Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) kwa magoli 35-10, ambapo hadi mapumziko Ikulu ilikuwa na magoli 15-6; nayo Wizara ya Mambo ya Ndani yenye mfungaji mrefu zaidi ya futi 7 waliwafunga Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini kwa magoli 74-4, hadi mapumziko Mambo ya Ndani walikuwa na magoli 36-2; Nayo Wizara ya Nishati ilipata ushindi wa chee wa magoli 40 na pointi mbili baada ya TARURA kushindwa kuingiza timu kiwanjani.
Nayo Hazina waliwachapa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa magoli 50-20, hadi mapumziko washindi walikuwa na magoli 24-7; wakati Shirika la Umeme nchini (TANESCO) waliwashinda Kongwa DC kwa magioli 41-4. Hazina walikuwa na magoli 24-3; huku UDOM wakiwachezesha kwata Mzinga kwa kuwafunga magoli 30-14, washindi walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 17-6; na Ikulu tena waliwafunga wadogo zao wa Wizara ya Maji kwa magoli 27-12. Ikulu walikuwa na magoli 12-5 hadi mapumziko. huku TRA waliwapeleka puta TARURA kwa magoli 36-12, ambapo hadi mapumziko washindi waliongoza kwa magoli 15-4.
Katika mchezo wa soka timu ya Uchukuzi SC waliwaliza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa bao 1-0 lililofungwa na Hussein Mwingira katika mchezo mwingine uliochezwa kwenye uwanja wa Kilimani Park; wakati timu ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini walimpata kibonde wao timu ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) na kuwafunga magoli 6-0 yaliyofungwa na Mponji Mhagama, Michael Gunem, Omary Kido, Simon Mng’ong’osi na Habibu Kilango kafunga mawili
Nayo timu ya TRA iliwafunga Manispaa ya Temeke ya Jijini Dar es Salaam kwa goli 1-0 lililofungwa na Isaya Laizer, ambapo mchezo huu umefanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, wakati timu za Wizara ya Afya na Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa zimetoka sare ya bao 1-1, nazo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimetoshana nguvu na Wizara ya Maji kwa kutoka sare ya mabao 2-2 kwenye uwanja wa Kilimani Park.
Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba kwa upande wanaume timu ya TARURA waliwashinda Tume ya Utumishi wa Walimu kwa mvuto 1-0; huku kwa wanawake timu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) waliwavuta Wizara ya Maji kwa mivuto 2-0; huku Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini wakiwavuta Wizara ya Afya kwa mivuto 2-0; nayo Ofisi ya Waziri Mkuu wakipata ushindi wa hee baada ya wapinzani wao TARURA kuingia mitini.
Michuano hiyo inayoshirikisha 41 kutoka kwenye Wizara, taasisi za umma na makampuni binafsi inatarajiwa kufikia kilele tarehe 30 April, 2022 inakaulimbiu ya “Michezo ni Afya na huamsha ari ya Kazi, Cheza, Chanja na Jiandae kuhesabiwa kwa Maendeleo ya nchi” inaendelea leo kwa kumaliza mechi za hatua ya makundi.
MWISHO