MKUU wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batlda Burian anatarajiwa kufungua Maadhimisho ya wiki ya Elimu Aprili 25, 2022 Wilayani Igunga Mkoa wa Tabora.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 19, 2022 jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Miradi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Alistidia Kamugisha amesema Maadhimisho hayo yatafungwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa Aprili 29, 2022 mkoani humo.
“Mkoa wa Tabora umechaguliwa kufanyiwa maadhimisho ya Juma la Elimu kwa lengo la kuungana na wenyeji kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kuhamasisha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wote,” alisema Bi. Kamugisha.
“Tunatambua juhudi mbalimbali zinazoendelea mkoani huko kwa lengo la kufanikisha upatikanaji wa elimu bora kwa wote lakini si vibaya pia na TEN/MET kama mtandao wa elimu wa kitaifa kushirikiana pamoja nao ili kuongeza nguvu zaidi na kufikia malengo.” Amesema Alistidia
Aidha ameongeza kuwa Maadhimisho ya wiki ya Elimu yameendelea kuchechemua maendeleo ya elimu kwenye mikoa na wilaya husika ambazo yamekwisha fanyika.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali wenye nia njema, wapenda elimu kuungana na TENMET pamoja na Serikali ya Mkoa wa Tabora, wilayani Igunga katika umaliziaji wa ujenzi wa bweni la wanafunzi wa shule ya Msingi Igunga ili kuongeza ulinzi kwa watoto na kuboresha mazingira ya kujifunzia ili asiachwe yeyote nyuma katika kupata elimu.
Amesema ili kufanikisha tuma mchango wako kwa namba hizi: Vodacom 0743 001 393 au Tigo 0678 280 859 Tanzania Education Network.
Maadhimisho yatahusisha shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo; kutembelea baadhi ya shule, kuendesha mikutano na kushiriki kazi za maendeleo ya jamii hasa mashuleni, kutakuwa pia na kongamano la elimu kimkoa lenye lengo la kuangazia kwa mapana changamoto za kielimu mkoani hapo na namna ya kuzitatua.
Maadhimisho hayo yataongozwa na kauli mbiu “Tuwekeze katika Elimu, kwa Elimu Bora na ujumbe “Elimu Kwanza”.
Maadhimisho haya maarufu kwa jina la Gawe, ikiwa ni kifupi cha maneno ya Kiingereza (Global Action Week of Education) yamekuwa yakifanyika kila mwaka duniani kote tangu mwaka 2003, yakilenga kuwaleta pamoja wadau wa elimu nchi mbalimbali kujadili na kufanya jitihada za pamoja kuhakikisha wanatatua na kupunguza changamoto zinazofanya watoto wasijifunze ipasavyo wawapo shuleni.