Na Selemani Msuya, Nanyumbu
UAMUZI wa Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kupeleka mradi wa maji katika kijiji cha Namijati, Kata ya Mkonono wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara, umetajwa kuwa utaboresha ndoa nyingi ambazo zilikuwa hatarani kuvunjika.
Hayo yamesemwa na wananchi wa kijiji cha Namijati wakati wakizungumza na waandishi wa habari ambao wametembelea miradi inayotekelezwa na RUWASA kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, kwa fedha za mkopo usio na riba wa Sh.trilioni 1.3 za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Zubeda Hassan (50), amesema hadi sasa hawajaamini kuwa kijiji chao kimepata maji yanayotoka kwenye bomba, kwani kwa miaka yake 50 ya kuzaliwa hajawahi kuona huduma kama hiyo.
Zubeda amesema kwa miaka mingi wamekuwa wakitumia muda mrefu kutafuta maji maeneo ya mbali kama Mnala, Masuguru, Nanyumbu na Mto Ruvuma, hali ambayo ilikuwa inakwamisha shughuli za uzalishaji na ndoa zao kuwa hatarini kuvunjika.
“Mimi nina miaka 50 hapa nilipo, sijawahi kuona bomba la maji hapa kijijini, hata mpaka sasa hatuamini labda siku yakitoka ndio tutaamini.
Tumekuwa tukisukuma madumu nane na mimba juu, huku tumeacha waume zetu au wao wametuacha, hii tunavunja haki za ndoa. Lakini mbaya zaidi unaondoka saa kumi alfajiri unarudi saa kumi jioni, hivyo hakuna shughuli nyingine ya uzalishaji inafanyika. Ila kwa sasa tunarajia kupumua,” amesema.
Mwana mama huyo amesema anashukuru RUWASA na Rais Samia Suluhu Hassan kuwakumbuka kwa kuwa wao walikuwa gizani katika huduma ya maji.
Naye Ustadh Ahmad Rukwekwe (37), amesema ujio wa maji kijijini kwao kutaamsha shughuli nyingi za uzalishaji, hivyo uchumi utakuwa.
“RUWASA wametuondolea adha ya kulala visimani kutafuta maji, hali ambayo ilikuwa inayumbisha ndoa zetu, pia uzalishaji utaongezeka. Ila pia kupitia maji hayo wanakijiji wataongeza kasi ya kufanya ibada zaidi,” amesema.
Rukwekwe amesema wamejipanga kulipia tozo za maji kwa kuwa wanajishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara.
Abasi Yassin amesema pamoja na mradi huo kuwapatia maji wanakijiji, pia vijana wengi wamepata kazi na kulipwa malipo sahihi.
“Kabla ya maji hajatoka, tumeshaanza kunufaika kwa kupewa kazi za kuchimba mitaro, kujenga tenki na nyingine, namshukuru Rais Samia kwa kutuletea mradi huu,” amesema.
Hamisi Mamboleo amesema kinachotokea kijijini kwao kwa kupata maji safi na salama ni maajabu ambayo hawakutarajia kuyaona kwa siku za karibuni.
“Kwa miaka mingi tunasikia huko Kaskazini, Magharibi na Mashariki mwa Tanzania wanafurahia huduma za maji, afya, ujenzi na nyingi, ila sasa na sisi tumekumbukwa. Kiujumla ili kauli kuwa Rais Samia anaupiga mwingi na sisi tumethibitisha,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Namijati, Ally Mussa amesema wao kama kijiji wanashukuru kwa Serikali na RUWASA kuwakumbuka na kuahidi kulinda ili uwe endelevu.
Mussa amesema mradi huo utanufaisha zaidi ya kaya 500 kijijini hapo, hali ambayo itachochea shughuli za maendeleo kukua.
Akizungumzia faida za miradi ya maji wilayani Nanyumbu, Ofisa Maendeleo ya Jamii (CSO) RUWASA, Daruana Mbacha amesema miradi hiyo ikamilika itaondoa changamoto nyingi na kuchochea maendeleo.
Mbacha amesema adha ya maji Namijati ilipelekea wakina mama wanaenda kujifungua kwenda na maji hospitali, hali ambayo sio sawa.
“Sisi kama CSO tunaamini upatikanaji wa maji Namijati unaenda kuondoa kero nyingi kama wakina mama wajawazito kwenda na maji hospitali,” amesema.
Mhandisi Crila Bayo kutoka RUWASA Nanyumbu amesema mradi huo unagharimu zaidi ya Sh.bilioni 1.35 na utanufaisha wakazi 3,328 wa kijiji cha Namijati na Mitumbatu.
Bayo amesema mradi huo ambao unatekelezwa na Kampuni ya Ukandarasi ya Caton Traders utaweza kuzalisha lita 15,800 kwa saa.
“Kazi ambazo zinafanyika katika mradi ni kujenga matenki matatu ambapo hadi sasa imefikia asilimia 50, nyumba ya mashine na mlinzi asilimia 50, ununuzi wa mabomba asilimia 100, uchimbaji wa mitaro na kusambaza bomba asilimia 15, kujenga vituo Namijati asilimia 100, Mitumbatu asilimia 90,” amesema.
Mhandisi huyo amesema kutakuwa na matenki matatu ambapo moja litakuwa na uwezo wa kupokea lita 100,000, 50,000 na 10,000 na kwamba baadae maji yatasambazwa kwa vijiji vingine.
Bayo amesema ujenzi wa mradi huo unaenda kuwakomboa wananchi wa vijiji hivyo ambao wamekosa maji safi na salama kwa miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania, huku akisisitiza kuwa Nanyumbu itafikia lengo la asilimia 85 ya maji vijijini.
Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Bahati Makuani amesema watajitahidi kumaliza kazi kwa wakati, pamoja na kuwepo na changamoto ya barabara hasa eneo la Mitumbatu.
Makuani amesema watatekeleza miradi wanayopewa na Serikali kwa ufanisi ili wasimuangushe Rais Samia ambaye ametambua umuhimu wao.
Naye Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mtwara, Primy Damas amesema mkoa huo unatekeleza miradi ya ustawi katika majimbo tisa ambapo hadi sasa wamefikia asimilia 50 ya utekelezaji.
“Mkoa huu una wilaya tano ambapo miradi ya ustawi inatekelezwa majimbo mawili ya Wilaya ya Mtwara ambayo ni Nanyamba na Mtwara DC, Newala mawili, Masasi matatu, Nyanyumbu na Tandahimba kuna majimbo mawili.
Miradi hii tisa inagharimu Sh.bilioni 5.37 na ikikamilika itaweza kuhudumia watu 65,000 na kuongeza asilimia ya upatikaji maji kuwa asilimia sita, hivyo tutatoka asilimia 62 ya upatikanaji maji hadi asilimia 68,” amesema.
Mhandisi Damas amesema pia wanatekeleza miradi ya lipa kwa matokeo chini ya mfuko wa maji ambayo pamoja na miradi mingine ikikamilika watafikia asilimia 75 ya upatikanaji wa maji.
Meneja huyo alisema pia kupitia mipango mbalimbali ya mkoa na wizara wanatarajia kupitia mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2025 lengo la maji vijijini asilimia 85 litafikiwa.
Mhandisi huyo ametoa wito kwa wananchi ambao miradi inatekelezwa katika vijiji vyao kutunza miundombinu hiyo ili iwe endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.