Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo (kulia), akipeana mkono na Mlezi wa Kituo cha Matumaini Sista Maria Peter baada ya kukabidhiwa msaada wa shilingi milioni tatu na vyakula, wakati Wizara yake na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar zilipotoa misaada hiyo, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo (kulia), akimkabidhi Bi. Rukia Khamis Abdalah msaada wa shilingi milioni tatu na vyakula, wakati Wizara yake na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar zilipotoa misaada hiyo, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo, akiwa katika picha na Watoto wa kituo cha Rahma kilichopo Chang’ombe, jijini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Divisheni ya Utumishi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Hamza Mkuwi Hamza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo, akiwa katika picha na Watoto wa kituo cha Matumaini kilichopo Mihuji, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano, WFM, Dodoma)
**********************
Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Serikali imewataka walezi wa watoto wenye mahitaji maalumu kufanya kazi hiyo kwa bidii na kwa upendo kwa kuwa wanalisaidia Taifa katika kuwapatia elimu, maadili na kupunguza watoto wa mitaani.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango huduma za Hazina, Bi. Jenifa Omolo, wakati Wizara yake na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango walipotoa misaada yenye thamani ya shilingi milioni tisa, vyakula na vinywaji katika Vituo vya Watoto wenye mahitaji maalumu vya Rahma, Cheshire na Matumaini.
Bi. Omolo alisema kuwa kazi zinazofanywa katika vituo hivyo Serikali inazitambua kwa kuwa ni kazi zinazohitaji upendo mkubwa ambao Mungu ameweka katika mioyo ya walezi wa watoto hao.
“Msaada huu tumeutoa kama Wizara kwa kutambua umuhimu wenu kwa kuwa watoto hao msinge wakusanya hapa inawezekana wasingepata nafasi ya kulelewa na kupata elimu na maadili mema, ikizingatiwa kuwa hawa ni viongozi wa kesho”, alieleza Bi. Omolo.
Alisema lengo la Wizara yake ni kufurahi pamoja na kuwatia moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwasaidia Watoto katika mahitaji yao ambayo wangeyapata kwa wazazi wao.
Aidha, ameupongeza uongozi wa vituo hivyo kwa kazi kubwa ya kuwalea watoto na kuwataka waendelee kuwa mama na baba kwa kuwafundisha elimu ya dini na kupata masomo mengine yatakayo waongezea ujuzi na maarifa.
Bi. Omolo pia amewaasa Watoto katika vituo hivyo kuwa waadilifu, wasikivu kwa walezi wao na kuzingatia masomo.
Kwa upande wake Mlezi wa Kituo cha Rahma, Bi. Rukia Khamis Abdalah, ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar kwa kitendo hicho cha kutoa misaada ambacho amekitaja kuwa ni ibada kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na wamefanya biashara na Mwenyezi Mungu na atawalipa baada ya maisha ya hapa Duniani
Naye Mlezi wa Kituo cha Matumaini Sista Maria Peter, amesema kuwa Watoto wanaolelewa katika kituo chake wanapatikana kupitia Maafisa ustawi wa jamii, ambapo maafisa hao wanapopata watoto wanatoa taarifa na kuomba nafasi ya kuwalea katika kituo, pia ameshukuru kwa msaada huo kwa kuwa watoto wanafarijika kwa kuuona upendo.