UJENZI wa Ofisi ya Kanda ya Kati ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ambao umebuniwa na unajengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Jijini Dodoma, kwa sasa umefikia asilimia 50 katika ujenzi ambapo Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Mshauri Mtogomi anasema ujenzi huo unatarajiwa kumalizika baada ya miezi mitatu.
“Katika mradi huu kazi kubwa imefanyika na kwa sasa tuko katika hatua ya kuezeka na kazi zingine ndogo za kumalizia, na kwa hatua hii tuliyofikia hatuna kazi kubwa tena mbele yetu na tunatarajia kumaliza baada ya miezi mitatu” amefafanua, Mhandisi Mtogomi
Aidha ujenzi huo umehusisha vitu vinne ambavyo ni ujenzi wa jengo zima, kibanda cha mlinzi ambacho kimekamilika kwa asilimia 30, uzio (Fence) imekamilika kwa asilimia 80 pamoja na mazingira ya nje kwa ujumla. Kwasasa ujenzi upo katika hatua ya uezekaji wa jengo zima.
Ujenzi ulianza mnamo mwezi Juni 2021 na ulitarajiwa kumalizika mnamo mwezi Februari, 2022 lakini kutokana na changamoto mbalimbali za ujenzi jengo hilo halijakamilika kwa muda uliopangwa.
Changamoto ambazo TBA imekumbana nazo na ambazo zimepelekea kutokumaliza mradi huu kwa wakati, ni pamoja na mfumuko wa bei wa vifaa vya ujenzi, hali ya hewa pamoja na upatikanaji wa marighafi ikiwemo Saruji. Na changamoto hizo zimeendelea kutatuliwa kadri inavyowezekana.