********************
Na Mwamvua Mwinyi, Dutumi
April 16
WATU sita wakazi wa Kitongoji cha Kigogo, Kijiji Kimara misale Kata ya Dutumi Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, wameliwa na mamba wakichota maji kwenye Mto Ruvu.
Baadhi ya wakazi wakizungumzia suala hilo, kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo ,akiwa kwenye kitongoji hicho akiwemo Said Kikwembe alisema wakazi hao wamekumbana na kifo hicho wakichota maji kwenye Mto Ruvu, unaopita maeneo yao hali inayowapa wakati mgumu.
“Hapa kwetu tumepatwa na misiba ya ndugu
zetu sita, ambao wameliwa na mamba miili mingine haijapatikana kabisa, tatizo hill linachangiwa na kukosekana kwa huduma ya maji,” alisema Kikwembe.
Nao Hamisi Maisha na Ashura Mkwayu walielezea ukubwa wa changamoto hiyo huku wakiiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia uwezekano wa kuwavuna mamba hao ili kuwapatia amani wakazi hao.
“Hapa hatuna amani kutokana na wanyama hao kushamili kwenye mto huo, ambao kwetu ndio tegemeo kubwa la kupatia maji tumekuwa hatuna amani huku tumipoteza wenzetu walioliwa na mamba,” alisema Ashura.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Salum Bong’o alisema kuwa katika mkasa huo wa mamba nae amempoteza Baba yake aliyeliwa na mamba miezi michache iliyopita, huku akimuomba Mbunge Mwakamo asimamie kikamilifu mradi wa maji unaoendelea kijijini Kimara Misale ili uwafikie Kigogo.
“Maji hapa Kigogo ni tatizo kubwa ndio linalosababisha vifo vya ndugu zetu, tunakuomba Mbunge huo mradi wa maji unaoendelea Makao Makuu ya Kijiji chetu Kimara Misale uharakishwe kisha utufikie na huku kwetu,” alisema Bong’o.
Akizungumza na wakazi hao Mwakamo kwanza aliwapa pole kwa matukio hayo, huku akizungumzia kasi ya zoezi la Mradi maji unaoendelea kijijini humo sanjali na Umeme imiwemo miundombinu ya barabara.
“Kuhusu barabara kama mnavyoona Mkandarasi yupo eneo la mradi, ujenzi wa Makaravati unaendelea kwa kasi isipokuwa changamoto itayosababisha kupunguza kasi ni hii mvua inayoendelea sasa,” alisema Mwakamo.
Kijiji cha Kimara Misale kwa miaka mingi kiliitika Jimbo la Kisarawe, ambapo kimekuwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa vyumba vya madarasa, maji, umeme na barabara ambapo kwa sasa sekta ya elimu vimejengwa vyumba zaidi ya saba.