Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Watumishi wa Mahakama nchini kuwa na desturi ya kufanya tathmini ya huduma wanazotoa kwa jamii ili kujua kama zinakidhi matarajio ya wananchi ya upatakanaji wa huduma ya haki kwa wakati.
Akizungumza jana tarehe 14 Aprili, 2022 jijini Arusha wakati akifunga Kikao kazi cha Mapitio ya Mpango Mkakati wa pili wa Mahakama wa 2020/2021-2024/2025 na Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama awamu ya pili, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa kwa kufanya hivyo utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa uboreshaji wa huduma za Mahakama utafanikiwa.
“Moja ya mambo muhimu ya kuzingatia katika utekelezaji wa Mpango Mkakati ni kujua au kujiuliza wewe kama Mtumishi ni nini unachokitoa katika jamii, je unatoa huduma kwa uwazi, je huduma unayotoa inafikika kwa wananchi na je haki unayotoa ni ya kiwango gani? Hivyo ni muhimu kuzingatia haya ili kazi iweze kufanyika kwa ufasaha,” amesema Mtendaji Mkuu.
Aidha, Prof. Ole Gabriel pia ametoa rai kwa Watumishi kuacha tabia ya kulaumiana katika utekelezaji wa majukumu badala yake kufanya kazi kama timu moja na hatimaye kutoa mrejesho wa masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma za Mahakama.
“Tusipende kulaumiana, tuwe na tabia ya kutoa mrejesho wa hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati na Mradi wa Uboreshaji wa huduma za Mahakama, kwa kufanya hivi tutafanikiwa,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.
Kadhalika, Mtendaji huyo aliongeza kwa kubainisha baadhi ya mambo yanayokwamisha utekelezaji wa Mipango Mikakati mingi ambayo ni pamoja na ukosefu wa watu wenye fikra kubwa (great minded people), kutokuwa au kukosa umoja ‘team spirit’ miongoni mwa watekelezaji wa Mradi pamoja na Uongozi kutoshiriki katika maandalizi ya Mpango Mkakati.
Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewataka Wamiliki wa Maeneo ya Utekelezaji wa shughuli za Mradi (Strategic Objective Owners) kuwa na umiliki wa dhati wa maeneo yao na vilevile kutoa ushirikiano kwa Kitengo cha Uboreshaji wa Huduma za Mahakama (JDU) ambacho kinaratibu utekelezaji wa shughuli zote za Mradi.
“Napenda kuwapongeza Waandaaji wa kikao hiki (JDU) pamoja na Washiriki wa Kada zote walioshiriki katika kikao kazi hiki, kazi iliyofanyika ni kubwa. Hivyo niwatake ‘SO-Owners’ kumiliki maeneo yenu pamoja na kutoa ushirikiano kwa Kitengo cha Uboreshaji wa Huduma za Mahakama (JDU) kwa kuwasilisha taarifa zinazotakiwa na mengineyo,” amesema Mhe. Chuma.
Mpango Mkakati wa Pili wa Mahakama (2020-2025) utatekelezwa kwa kiasi kikubwa na nyongeza ya Mkopo wa Benki ya Dunia wa Dola Milioni 90 baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya Mradi uliokuwa na matumizi ya Dola milioni 65 ambazo Benki ya Dunia iliikopesha Serikali ya Tanzania kwa matumizi ya kuboresha huduma ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Kikao kazi hicho kilichohusisha jumla ya Washiriki wapatao 250 wakiwemo Majaji, Wasajili wa Mahakama, Watendaji wa Mahakama na baadhi ya Watumishi wa Kada mbalimbali wakiwemo wa ngazi za chini (Wasaidizi wa Ofisi, Katibu Muhtasi, Watunza Kumbukumbu na wengineo) kililenga kufanya tathmini ya Mafanikio, changamoto ya Mradi wa awamu ya kwanza pamoja na mapitio ya awamu ya pili ya Mradi.