Mkandarasi wa Kapumuni ya Ujenzi Nipo Afrika, Lington Mushi akizungumza na waadnishi waliotembelea , Mradi wa Maji Kwambe wilyani Nyasa mkoani Ruvuma.
Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Civito, Mhandisi Stanley Mlelwa akiwaeleza waandishi wa habari namna miradi ya maji ya Ustawi inavyowarejesha kwenye chati ya ukandarasi.
Mkandarasi Geofrey Karubwaga anayesimamia ujenzi wa Mradi wa Maji Amani Makoro wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma akielezea utekelezaji ulipofikia.
Fundi Lucas Ngayele akichota kokoto kwa ajili ya ujezni wa Mradi wa Maji Kwambe wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Fundi Bosco Kapinga akielezea namna Mradi wa Maji wa kijiji cha Daraja Mbili unavyomnufaisha kiuchumi.
Fundi Remidus Komba akielezea namna Mradi wa Maji wa kijiji cha Daraja Mbili unavyomnufaisha kiuchumi.
Zamda Zuberi na Asha Nasibu wakielezea namna ujenzi wa Mradi wa Maji Daraja Mbili unavyowanufaisha kwa kipato.
……………………………………………………..
Na Selemani Msuya, Ruvuma
WAKANDARASI na mafundi wazawa wanaotekeleza miradi ya maji kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwaamini na kuwapatia miradi hiyo.
Shukurani hizo zimetolewa na makandarasi na mafundi wanaotekeleza miradi ya Uviko-19 inayosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), katika Wilaya ya Nyasa, Mbinga na Tunduru mkoani Ruvuma.
Wakizungumza na waandishi waliotembelea Mradi wa Maji katika Kijiji cha Kwambe wilayani Nyasa, Mkandarasi Elington Moshi wa Kampuni ya Nipo Africa Engineering Limited amesema uamuzi wa Serikali kuwapatia zabuni wakandarasi wa ndani ni wa kuoongezwa na kuendelezwa.
Moshi amesema amejipanga kutekeleza miradi hiyo ya maji kwa ubora ambao utaifanya Serikali kuwapatia kazi nyingi wakandarasi wa ndani kila mara.
“Kampuni yetu ya Nipo Africa itahakikisha inatekeleza miradi kwa ubora na ufanisi, ili mradi uweze kudumu kwa muda mrefu na thamani ya fedha ionekane,” amesema.
Naye Mkandarasi Geofrey Karubwaga ambaye kampuni yake inatekeleza Mradi wa Maji Amani Makoro wilayani Mbinga, alisema hadhi ya wakandarasi wa ndani imeanza kurejea, hivyo watahakikisha wanaacha alama nzuri.
“Miradi hii ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na nchi, hivyo jukumu letu wakandarasi wazawa tunaitekeleza kwa kiwango bora ambacho kitakuwa endelevu. Niahidi kutomuangusha Rais Samia,” amesema.
Kwa upande wake Mkandarasi Stanley Mlelwa wa Kampuni ya Ukandarasi ya Civito, amesema wao wanatekeleza mradi wa maji Daraja Mbili na Kazamoyo wilayani Tunduru ambapo hadi sasa wamefikia zaidi ya asilimia 70 ya utekelezaji.
“Napenda kumshukuru Rais Samia kuturejeshea fursa hii ya utekelezaji wa miradi kwani kipindi cha miaka ya nyuma tumepitia wakati mgumu, kazi kama hizi walipewa mafundi wa kawaida. Ninamuahidi kuwa hatutamuangusha,” amesema.
Mlelwa amesema utekelezaji wa miradi hiyo umekuwa na ufanisi kwa kuwa RUWASA wamekuwa wakitimiza majukumu yao kwa weledi.
Nao mafundi John Komba, Lucas Ngayele, Bosco Kapinga na Remidus Komba wamesema miradi hiyo ya maji ambayo inatekelezwa kwenye vijiji vya mkoa wa Ruvuma mbalimbali imeweza kuwapatia kipato hali ambayo inasaidia wao kuhudumia familia zao vizuri.
Mafundi hao walimuomba Rais Samia na Serikali yake kuwapatia miradi mingine ili waweze kupata kazi za kufanya ambazo zitaweza kuwaondolea changamoto mbalimbali za kimaisha.
Naye Zamda Zuberi na Asha Nasibu wanajishuhulisha na kupika chakula cha mafundi, wamesema mradi huo umewawezesha kubadilisha maisha yao kwa kujipatia kipato hivyo kufanikisha majukumu yao ya kifamilia kama kununua daftari, kalamu, mboga na mengine muhimu.
Wakina mama hao wanasema kupitia mradi huo wamekuwa wakiwapikia mafundi ambao wanatekeleza mradi huo katika kijiji cha Daraja Mbili.