Meneja wa shamba kutoka ASA -Tengeru,Benson Minji akizungumza na waandishi wa habari pamoja na watafiti waliotembelea kituo hicho jijini Arusha (Happy Lazaro).
**************************
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Wakulima washauriwa kulima kwa wingi mchicha aina ya Poli ambao una faida kubwa ikiwemo mbegu zake kutumika Kama unga wa lishe kutokana na virutubisho vingi vilivyopo kwenye unga huo.
Hayo yamesemwa na Meneja wa shamba kutoka Wakala wa mbegu za kilimo (ASA )-Tengeru,Benson Minji wakati akizungumzia na waandishi wa habari pamoja na watafiti walipotembelea kituo cha Tari-Tengeru kujionea shughuli mbalimbali ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania (COSTECH).
Minji amesema kuwa, mchicha huo ambao unajulikana Kama mchicha wa maajabu , mbegu zake husagwa na kupatikana unga wa lishe ambapo una uwezo wa kukomaa ndani ya siku 21 huku majani yake yakitumika kama mchicha huo ukiwa na kiwango kikubwa Cha protini.
Ameongeza kuwa, mbegu za mchicha huo zinasaidia Sana kuboresha afya ya watoto kutokana na virutubisho vingi vilivyopo katika unga wake .
“Nawashauri wakulima walime kwa wingi mchicha huu wa Poli kwani una faida nyingi na kuna zaidi ya makampuni 50 Arusha wamechukua mbegu hizo na kwenda kuzalisha pamoja na kusambaza hapo tunaona ni jinsi gani uhitaji wa mchicha huo ulivyo juu,hivyo wakulima wetu wachagamkie fursa hiyo kwani unakomaa ndani ya siku 21 tu”amesema Minji.
Ameongeza kuwa, kwa msimu huu wameweza kuzalisha mbegu za mchicha huo wa Poli kilo 192 ambapo mbegu zake zikisangwa unga wake unatumika kwa ajili ya lishe ya watoto,wagonjwa kutokana na kiwango kikubwa cha Zinc kilichopo ndani ya unga huo.
“Mfumo mzima wa mbegu umekuwa ukianzia kwa watafiti kutoka Tari ambapo sisi Kama wakala wa mbegu za kilimo ASA ndo wazalishaji wa mbegu hizo baada ya kufanyika tafiti, na makampuni yanayonunua yameonekana kupata faida kubwa kupitia mchicha huo kulingana na uhitaji mkubwa uliopo “amesema.
Nawashauri wakulima wachangamkie fursa ya kulima mchicha huo ambao una faida kubwa na unakomaa ndani ya siku chache huku mbegu zake zikiwa na faida kubwa.