Na Dotto Mwaibale, Singida
AFISA Mtendaji wa Kata ya
Dung’unyi wilayani, Ikungi mkoani Singida Yahaya Njiku ametoa onyo kali
kwa Wazazi na Walezi wenye tabia ya kuwarubuni watoto wao waache kwenda shuleni
huku wakitoa sababu mbalimbali ikiwemo ya kutaka kuwaoza.
Njiku alitoa onyo hilo jana
alipokuwa akizungumza na wazazi na wanafunzi wakati wa ziara yake ya
kukagua miradi katika Shule ya Sekondari Munkinya ilioyopo katika kata hiyo.
” Hivi karibuni kumezuka tabia
ya baadhi ya wazazi kuwarubuni watoto wao waache shule ili wabaki
nyumbani kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuwaoza na wengine wanaambatana
na watoto wao mpaka ofisi za Serikali za Vijiji na kata ambako wamekuwa wakitoa
madai eti watoto wao hawataki shule hivyo wanaomba wafutwe” alisema Njiku.
Njiku alisema mzazi au mlezi atakaye
bainika akifanya hivyo hatamvumilia atamkamata na kumfikisha kwenye vyombo cha
dola na katika jambo hilo hata kuwa na huruma na mtu.
Alisema ni jambo la ajabu kwa mzazi
na mlezi kufanya jambo hilo kwani Serikali imetumia fedha nyingi kuboresha
miundombinu mashuleni ili watoto wapate elimu katika mazingira bora alafu
anatokea mzazi akidai anataka mtoto wake aachishwe shule.
” Itakuwa Serikali ya ajabu
ambayo itaukubali upuuzi huo nasema ole wake mzazi tukakaye mbaini
akifanya hivyo” alisisitiza Njiku kwa ukali.
Alisema ni wajibu wa wazazi na
walezi kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya
elimu wawapo shuleni na nyumbani lakini si kwa kuwarubuni kuacha shule.
Njiku alitumia nafasi hiyo
kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani
kwa kuwapatia kiasi cha Sh. Milion 40 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili
katika shule hiyo ambapo aliwasisitiza wanafunzi hao kusoma kwa bidii.