Mkuu wa wilaya ya Karatu,Dadi Kolimba akikata utepe ishara ya uzinduzi wa mradi huo wa miaka mitano unaotekelezwa na shirika la SOS Children’s Villages
Mkurugenzi wa shirika la SOS Children’s Villages Tanzania,David Mulongo akizungumza katika uzinduzi huo jijini Arusha.(Happy Lazaro)
…………………………………………….
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Zaidi ya watoto 102,000 wanaotoka mazingira magumu wanatarajiwa kunufaika kielimu,afya, lishe na haki za msingi kwa ujumla na kuweza kuondokana na changamoto mbalimbali za maisha .
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi wa shirika la kutoa malezi kwa watoto SOS Tanzania ,David Mulongo katika uzinduzi wa upanuzi wa mradi wa ulinzi wa watoto, mradi unaoshirikisha Serikali na shirika la SOS.
Aidha mradi huo wa miaka mitano unatekelezwa katika halmashauri ya Arusha Dc,Meru, halmashauri ya jiji,pamoja na Karatu lengo kubwa likiwa ni kuwepo kwa malezi bora dhidi ya mtoto na kuweza kujenga uwezo wa kiuchumi kwa vijana ili waondokane na maisha hatarishi waliyokuwa wanaishi.
Mulongo amesema kuwa,shirika hilo limekuwa likilea watoto kuanzia miaka 0-24 ambapo zaidi ya watoto 700 wanaendelezwa kupitia vijiji vyao vilivyopo Zanzibar,Dar es Salaam ,Arusha na Mwanza na tayari zaidi ya vijana 50 walishafanikiwa na kuwa na shughuli zao za kufanya na kuweza kuanzisha maisha yao.
Ameongeza kuwa,shirika hilo limeweza kuwatafutia ufadhili vijana zaidi ya 30 ambao tayari wapo nje ya nchi baada ya kupata ufadhili kupitia shirika hilo huku lengo kuu likiwa ni kumtoa mtoto katika mazingira magumu anayoishi na kumtafuta mazingira bora na kuweza kupata haki zake zote za msingi.
“Tunatarajia kutoa kipaumbele katika kuwafikia watoto waishio mazingira hatarishi katika mikoa ya Dar es Salaam,Mwanza,Dodoma ,Mbeya na Arusha ambapo matarajio yetu ni kuhakikisha mkoa wa Arusha unakuwa wa mfano katika kuwahudumia watoto wanaotokea mazingira hatarishi”.amesema .
Naye Mkuu wa wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba akizungumza katika ufunguzi huo amelipongeza shirika hilo kwa shughuli kubwa wanayofanya ya kuhudumia watoto hao kwa zaidi ya miaka 10 sasa kwani inaleta manufaa mengi kwa ulinzi na uimarishaji wa mtoto.
“Nimesikia changamoto mlizozibaini wakati wa kufanya upembuzi wa mradi ikiwemo ukosefu wa mtaji kwa vijana,elimu ya ufundistadi, ukosefu wa elimu ya mama na mtoto, unyanyasaji was mtoto pamoja na jamii kutokuwa na elimu mbadala ,hivyo naombeni changamoto hizi zikawe ndo kipaumbele cha kuzitatua ili kuonyesha maana halisi ya kile mnachokifanya katika jamii.”amesema Kolimba.
Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha ,Dk . Sylvia Mamkwe amesema kuwa , shirika hilo limekuwa ni mkombozi hususani kwa mkoa wa Arusha kwani limekuwa likiwasaidia watoto wanaotokea mazingira magumu na kuweza kuwahudumia katika nyanja mbalimbali.
Amesema kuwa, utaratibu wanaotumia wa kuwatambua watoto hao katika familia zao kupitia watendaji wa maeneo husika ni mzuri kwani wao ndio wanaojua walengwa na changamoto wanazokabiliana nazo,huku akiwataka kuongeza bidii zaidi katika kuwafikia watoto wengi zadi.